Diwani: Wazee msirubuniwe na zawadi kuelekea Uchaguzi S/Mtaa

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 02:10 PM Jul 22 2024
Diwani Yona Ntunjilwa (wa pili kushoto), akimkabidhi viatu mjane Enere Soso, mkazi wa Mtakuja Kivukoni, Mbalizi, Mbeya Vijini. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa SAMAFO, Tabitha Bugali, akishuhudia tukio hilo.
PICHA: MPIGA PICHA WETU
Diwani Yona Ntunjilwa (wa pili kushoto), akimkabidhi viatu mjane Enere Soso, mkazi wa Mtakuja Kivukoni, Mbalizi, Mbeya Vijini. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa SAMAFO, Tabitha Bugali, akishuhudia tukio hilo.

DIWANI wa Kata ya Utengule Usongwe, Yona Ntunjilwa, amesema kuelekea uchaguzi serikali za mitaa mwaka huu, wazee hususan wanawake wasiwe tayari kurubuniwa na zawadi ndogo kutoka kwa wanasiasa.

Ntunjilwa aliyasema hayo mkoani Mbeya, mwishoni mwa wiki wakati tukio la kuwakabidhi watoto, wajane na wagane wa kata hiyo, msaada wa nguo lililoandaliwa na shirika la Sauti ya Mama Afrika Foundation (SAMAFO), kwa kushirikiana na wadau.

“Mwaka huu tuna uchaguzi wazee msirubuniwe huko nje kuelekea uchaguzi serikali ya wa mtaa. Wazee mjitokeze kupiga kura ya maoni na kura yenyewe.

“Kinamama nyie mna nguvu sana na usipowasemea yanayowahusu, umekwenda na maji. Wanawake wanaweza bila kuwezeshwa,” alisema Ntunjilwa.

Ntunjilwa aliwawakumbusha viongozi wenzake kwenye kata hiyo, kutambua mahitaji ya wakazi wao, kwa kuwatembelea huku akiwataka waliopewa msaada huo kuwa shukrani hata kama ni kidogo.

“Viongozi wa mtaa mnatakiwa kujua hali ya maisha ya wakazi wenu na kuweka utaratibu wa kutoa msaada hasa kwa wajane na wagane. Wazee kwenye jamii ni muhimu huonya, hufundisha.

“Tumejifunza leo kutokana na msaada wenu huu, uliotolewa kutoka kwa wadau na wenzetu na kuwakumbuka wakazi wa eneo letu. Ukiwatazama wazee hawa utabaini ni kati ya wanaohitaji msaada,” aliongeza.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa SAMAFO, Tabitha Bugali, alisema utaratibu wa kutoa msaada kwa makundi maalumu kama vile yatima na wazee ni endelevu, kwa kushirikiana na wadau wengine wenye malengo yanayofanana.

“Tumeshirikiana na wenzangu kutoka shirika la AMAWAMBE, Twende Wote Foundation (TWF), pamoja na Mary Gumbo, kutekeleza jambo hili ikiwa ni miongoni mwa shughuli tunazofanya kuigusa jamii,” alisema Tabitha.

Mary Gumbo, aliyekuwa mkuu wa dawati la jinsia Jeshi la Polisi Mbeya DC na kata hiyo, alisema kutoa msaada kwa kundi hilo ni umshukuru Mungu kudumu kazini kwa miongo kadhaa, hadi kustaafu Julai mwaka huu.

“Katika dawati nimeshirikiana na SAMAFO kutoa msaada kwa wajane, wagane ikiwamo sabuni, unaofikia takribani Sh. milioni moja. Hii ni shukrani kwa jamii na kushukuru hadi hapa nilipo leo ni mstaafu,” alisema Mary.