VIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo wamesema tatizo la ajira linatishia ustawi na amani ya nchi.
Wamedai kuwa janga la ukosefu wa ajira nchini linasababishwa na serikali kutekeleza sera mbovu zinazokausha ajira, zinazoweka mazingira mabovu ya watu wanaofanya shughuli zao za uchumi.
Kiongozi wa Chama hicho, Dorothy Semu, akiwa Manyoni mkoani Singida juzi katika awamu wa kwanza ya ziara ya kufikia majimbo 214, alisema serikali imeshindwa kutatua tatizo la ajira na kuweka mazingira wezeshi ya kujiajiri.
“Ukweli mchungu ni kwamba serikali imeshindwa kutatua tatizo la ukosefu wa ajira, zaidi ya watanzania milioni 3.5 wanaotafuta kazi, hawana kazi na hakuna matumaini ya mabadiliko labda kuiondoa CCM madarakani.
“Watu milioni 18.8 wanajishughulisha na kilimo, uvuvi na uchimbaji wakati huo hawana hakika ya ujira unaoeleweka,” alisema.
Alisema wimbi la watu wasiokuwa na ajira rasmi ni kubwa nchini na mazingira yao ya kazi sio mazuri. “Hawana hakika ya kipato, hawana pensheni, bima ya afya wala vivutio au misamaha ya kodi ili kukuza biashara zao,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Tanzania Bara, Isihaka Mchinjita, akiwa Songea mjini, alisema serikali haijaweka kipaumbele katika kushughulikia tatizo la ajira, licha ya kuwapo kwa mahitaji makubwa ya watumishi katika sekta ya elimu, afya na kilimo.
“Kila mwaka Tanzania inazalisha nguvu kazi ya watu milioni moja wanaohitimu kutoka vyuo vya elimu ya juu, vyuo vya ufundi, shule za sekondari na msingi.
“Lakini uwezo wa CCM kuzalishia ajira kwa mwaka ni watu elfu 70,000 tu. Hii ina maana kuwa CCM imejenga uchumi kilema usio zalisha ajira,” alidai Mchinjita.
Kuhusu upungufu wa watumishi, alisema sekta ya elimu kuna upungufu wa walimu 279,202 na watumishi wa afya 221, 998.
Alisema pamoja na upungufu huo, serikali haijaweka mkazo kuhakikisha sekta hizo zinapata wataalamu na watumishi, licha ya kuwapo kwa vijana waliosomeshwa kwa gharama kubwa, serikali ina waacha mtaani wanakuwa machinga, bodaboda na mamantilie.
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Ado Shaibu, alitaja mazingira kandamizi kwa vijana waliojiajiri na kuwapo kwa ajira zenye ujira mdogo kwamba, inawafukarisha vijana na kuwafaidisha watu wachache.
“Vijana walioamua kujiajiri katika biashara, huduma, uchimbaji pamoja kilimo wanakumbana na vikwazo vingi. Tumeshuhudia wamachinga wakiondolewa na kuhamisha sehemu zenye mzunguko mkubwa wa biashara.
“Wakitaka kuanzisha biashara masharti yake ni magumu, biashara zinafungwa. Wachimbaji wadogo wanaondolewa kwenye migodo kupisha wanaowaita wawekezaji,” alisema.
Shaibu alisema kuwa licha ya mchango wa sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji katika ajira, bado kilimo hakijawekewa mkazo na serikali hivyo, kukifanya kuwa mzigo kwa nguvu ya vijana.
Kiongozi Mstaafu, Zitto Kabwe, akiwa Buyungu Kigoma alisema CCM imetengeneza uchumi dumavu usiozalisha ajira na kutelekeza nguvu kazi za vijana kwa kuwafanya tegemezi.
Zitto alisema hali hiyo inaweza kusababisha ukosefu wa utulivu nchini.
“Kutokana na ukubwa wa tatizo la ajira nchini, CCM isifikirie kuwa Gen Z haiwezi kuibuka Tanzania, vijana wasiokuwa na ajira watakachoka na kujipanga kudai haki zao.
“Nguvu kazi ya watanzania milioni 33 ni watu milioni 3 pekee ndio walioajiriwa rasmi katika sekta za umma. Hili tatizo linazidi kuwa kubwa chini serikali ya CCM,’’alisema.
“Leo hii sio ajabu kumkuta mhitimu wa shahada akiwa machinga au dereva wa bodaboda. Hii ni kupoteza nguvu kazi ya taifa kwa kuwaingiza katika kazi wasizozisomea. Tunapoteza nguvukazi hii kwa sababu CCM imegota haina uwezo tena wa kuleta mabadiliko.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED