Inapotangazwa operesheni mambo haya ya saratani, tuungane kusaka

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 01:34 PM Oct 18 2024
Inapotangazwa operesheni mambo  haya ya saratani, tuungane kusaka
Picha:Mtandao
Inapotangazwa operesheni mambo haya ya saratani, tuungane kusaka

UGONJWA wa saratani upo katika maeneo mbalimbali ya mwili wa mwanadamu. Ni maradhi yanayowapata watu wa aina yoyote na hauchagui rika.

Ni ugonjwa ambao unatokana na visababisha mbalimbali. Baadhi ya jamii huhisi kuna saratani ya matiti na shingo ya uzazi.  

Ugonjwa wa saratani upo katika makundi mbalimbali, huku jamii inaweza kwa jumla kupata ugonjwa huo. Kuna saratani ya koo, saratani ya shingo ya kizazi, damu na saratani ya matiti.  

Katika kukabiliana na ugonjwa huo, serikali imekuwa ikitoa elimu kwa jamii ili isipate magonjwa hayo ambayo imeonekana kila mwaka yanaongezeka.  

Hivi karibuni serikali kupitia Wizara ya Afya, imeendelea kushirikiana na wadau kutokomeza ugonjwa huo nchini na serikali inatoa elimu kwa jamii, pamoja na kuhimiza upatikanaji wa chanjo, mathalan dhidi ya  saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana.  

Kwa kuwa ugonjwa huo umekuwa ukiongezeka kila mwaka, serikali imejipanga kupambana nayo kwa kuboresha mahitaji ya huduma hiyo katika hospitali na vituo vya afya.  

Waziri wa Afya, Jenister Mhagama, anasema hayo katika ufunguzi wa kituo cha saratani kilichoko katika Hospitali ya Shufaa iliyoko jijini Dar es Salaam, akinena: 

 "Ufunguzi wa kituo hiki utaongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani hapa nchini kwa kuwa tatizo la ugonjwa huo limekuwa likiongezeka hapa nchini," anasema.  

Anaongeza kuwa takwimu za saratani hapa nchini kwa mwaka 2022, zimeonyesha wagonjwa wapya wako 48,000 na kati yao waliogundulika asilimia 24.4 ni saratani ya mlango wa kizazi. 

 Anaongeza kuwa saratani ya tezi dume waligundulika asilimia 10.7, saratani ya matiti asilimia 10 na saratani ya koo asilimia 7.9 na saratani ya utumbo asilimia 4.9.  

"Saratani hizi zinachukuwa karibu nusu ya asilimia 42.2 ya wagonjwa wote wa saratani hapa nchini," anasema.  

Anaongeza kuwa saratani mbili zinaziathiri zaidi wanawake ni saratani ya mlango wa uzazi na saratani ya matiti ndio zinachukuwa theluthi moja ya wagonjwa wote wa saratani hapa nchini. 

 Anasema, kufuatia kuongezeka kwa saratani nchini, serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwamo utoaji wa elimu ya afya pamoja na kuimarisha huduma za uchunguzi wa saratani ya mlango wa uzazi katika hospitali ikiwamo na vituo vya afya hapa nchini.  

Anaongeza kuwa wajibu wao kama serikali ni uthibiti wa ubora na sio udhibiti wa sekta binafsi kukua, wataendelea kushirikiana na sekta binafsi kwa pamoja ili waweze kutoa huduma iliyo bora na salama kwa wananchi. 

Waziri anasema, ili kuongeza ufanisi katika huduma za uchunguzi. 

Pia serikali imeimarisha upatikanaji huduma za uchunguzi wa maabara na uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye huduma za radiolojia kwa kuimarisha upatikanaji vipimo vya kisasa ikiwamo vifaa; CT Scan 85 katika mikoa yote 26 nchini. 

Sasa cha muhimu kwetu site ni pale juhudi na hatua kama hizo zinachukuliwa na serikali kutetea nafasi ya afya zetu, sote tujitahidi katika nafasi yetu kuunga mkono katika namna mbalimbali, ikiwamo kujitokeza katikia chanjo na tiba. 

Pia, kila mmoja mwenyewe katika nafasi yake inapaswa kujitahidi kutambua na kuna fursa ya kijamii, huku ikitangaza katika namna mbalimbali kufuata hatua ya mafanikio katika eneo hilo.