Utumishi yaanika wataalamu sugu ukiukaji maadili kazini

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 02:00 PM Oct 18 2024
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Xavier Daudi.
Picha: Utumishi
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Xavier Daudi.

OFISI YA Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeanza kupokea tuhuma na malalamiko kuhusu kuwapo kwa viashiria vya mmomonyoko wa maadili kinyume na mila na desturi vinavyohusu vitendo vya mapenzi ya jinsia moja kwa baadhi ya watumishi wa umma.

Aidha, ofisi hiyo imepokea mrejesho kutoka kwa wananchi wanaohudumiwa kuhusu hali isiyoridhisha ya mavazi kwa watumishi wa umma.

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Xavier Daudi, aliyasema hayo jana jijini hapa kwenye ufunguzi wa kikao kazi baina ya ofisi hiyo, taasisi zinazosimamia maadili na mamlaka zinazosimamia maadili ya kitaaluma.

Alisema vitendo hivyo ni miongoni mwa vya kijinai kwa mujibu wa sheria za nchi, na kinyume cha maadili kwa mujibu wa miongozo ya utumishi wa umma.

“Tumieni kikao kazi hiki, kujadili na kubadilishana uzoefu ili kuja na mapendekezo ya namna sahihi ya kudhibiti vitendo hivi na namna sahihi ya kushughulikia masuala haya yatakapojitokeza katika maeneo yenu ya kazi kwa baadhi ya watumishi wanaohusishwa navyo ili kuepuka kuchafua taswira ya utumishi wa umma kwa ujumla,” alisema.

Pia alisema wamepokea taarifa za malalamiko mengi kutoka vyanzo mbalimbali, yatokanayo na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya utendaji na maadili ya kitaaluma katika utumishi wa umma yakiwahusisha baadhi ya watumishi wa kada za wauguzi, madaktari, walimu, maofisa utumishi, maofisa ardhi, wahasibu katika halmashauri, wataalamu sekta ya ugavi wa umeme na maji, pamoja na wahandisi wanaosimamia miradi ya maendeleo.

“Wajibu wa kusimamia maadili ya watumishi wa umma katika utumishi wa umma ni mtambuka ambalo kisheria liko chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mujibu wa kifungu cha 8(3)(e) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298,” alisema.

Aidha, aliwataka wajumbe wa kikao hicho kupitia Waraka wa Utumishi wa Umma Na. 6 wa mwaka 2020 kuhusu Mavazi kwa Watumishi wa Umma, ili kujengeana uelewa wa pamoja kupitia uzoefu watakaobadilishana. “Mtakaobadilishana uzoefu kuhusu utekelezaji wa waraka huo kwa watumishi walioko kwenye maeneo yenu, na muweze kuchukua hatua ipasavyo kwa wanaokiuka waraka husika ikizingatiwa kuwa, mwonekano wa watumishi wa umma wanapotoa huduma unabeba taswira ya taasisi, utumishi wa umma na serikali kwa ujumla,” alisema. 

Aliwahimiza kujenga uwezo wa watumishi kimaadili kupitia mafunzo ya maadili katika maeneo yao ya kazi na matumizi ya serikali mtandao katika utoaji wa huduma ili kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa maadili na kufanya utafiti mbalimbali wa kubaini hali ya uadilifu katika taasisi zao.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Usimamizi wa Maadili, Ally Ngowo, alisema wanatarajia kupokea taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha Septemba 2023 hadi Septemba 2024 katika maeneo yao kuhusu suala la maadili.

Alitaja mada watakayojadili kuwa ni umuhimu wa matumizi ya mfumo wa E-Mrejesho katika matumizi ya maadili ya utumishi wa umma.