Wachoma nyumba madai kulipiza kisasi mauaji bodaboda mwenzao

By Gideon Mwakanosya , Nipashe
Published at 03:05 PM Oct 18 2024
Wachoma nyumba madai kulipiza  kisasi mauaji bodaboda mwenzao
Picha:Mtandao
Wachoma nyumba madai kulipiza kisasi mauaji bodaboda mwenzao

WATU wanaodaiwa kuwa madereva wa bodaboda wanadaiwa kuchoma nyumba ya Adili Mpambula wa mtaa wa London, Kata ya Lizaboni, Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kumwua dereva mwenzao, Sharif Luambano, ambaye ni mkazi wa eneo hilo.

Chanzo cha mauaji hayo kinadaiwa kuwa ni deni la marejesho ya pikipiki kwa mkataba ambao ulikuwa umebaki miezi miwili kumalizika. 

Mbali na kuchoma nyumba hiyo, wananchi hao pia waliweka magogo kuzuia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwenda kuzima moto katika nyumba hiyo iliyokuwa inateketea. Baadaye jeshi hilo lilipita na kufika kwenye nyumba hiyo lakini ilikuwa imeshateketea. 

Akizungumza na mwandishi wa habari hii jana, Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ruvuma, Merania Nyambwinyo, alisema kuwa akiwa ofisini Octoba 15, mwaka huu, majira ya saa 5:00 asubuhi, alipokea taarifa ya nyumba kuteketea kwa moto, hivyo kujiandaa kwenda kwenye tukio hilo. 

Kamanda Nyambawinyo alisema walipofika jirani na eneo la tukio, ghafla waliona mbele yamewekwa magogo makubwa barabarani na waliposimama, walisikia sauti za watu wakisema gari la zimamoto lisifike kwenye eneo la tukio na hakuna mtu kuondoa magogo.

Hata hivyo, alisema baadaye walifanikiwa kuyaondoa magogo hayo kisha kupita na  askari walipofika kwenye eneo la tukio, walikuta nyumba yote imeteketea kwa moto.

Alisema nyumba hiyo yenye vyumba vitatu,  sebule na banda la vyumba vitatu nyuma na mali zote zilizokuwamo ndani, ziliteketea. 

Chanzo cha tukio hilo alisema ni madai kwamba Mpambula alimuua jirani yake kwa kumjeruhi kichwani na kumsababishia kifo kisha alikimbia na kutokomea kusikojulikana.

Alisema wananchi walilizuia gari la zimamoto kwa madai kuwa wamechoma nyumba hiyo kwa sababu mmiliki amemuua mwenzao.

Kutokana na tukio hilo, kamanda huyo wa zimamoto aliwashauri wananchi kuacha  kujichukulia sheria mkoni kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria. Alisema wananchi hao kama wasingeweka magogo hayo kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kuokoa baadhi ya mali zilizokuwamo ndani ya nyumba hiyo. 

Diwani wa Lizaboni, Odo Mbunda, alisema Luambano ambaye alikuwa Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Amani, aliuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na jirani yake Mpambula ambaye alikuwa anadai fedha za marejesho ya pikipiki waliyowekeana mkataba baada ya muda wa mwaka mmoja alipaswa kuendelea kumiliki pikipiki hiyo ambayo ilibaki marejesho ya miezi miwili. 

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Fadhili Mdemu, alisema Luambanioo kabla ya kufikwa na umauti, Oktoba 14, mwaka huu, majira ya saa 2:00 usiku, alijeruhiwa vibaya kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na Mpambula. Alisema baada ya kujeruhiwa, alipelekwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Ruvuma mjini Songea ambako alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu. 

Mdemu alisema mtuhumiwa alitoroka baada ya kutenda tukio hilo na kwamba juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Alisema kutokana na kitendo hicho, kundi la madereva bodaboda walijichukulia sheria mkononi kwa kuvamia nyumba ya Mpambula na kuchoma moto nyumba hiyo na kuteketea. 

Kamanda Mdemu alisema hakuna madhara yoyote kwa binadamu na kwamba upelelezi wa tukio hilo unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwasaka watuhumiwa wote waliohusika kuichoma nyumba hiyo na kuzuia gari la zimamoto lililokuwa linakwenda kufanya  uokoaji.