Viongozi wasisitizwa kutobagua watu katika kuwatumikia

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 04:41 PM Oct 18 2024
KATIBU wa Idara ya Oganaizesheni ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Issa Gavu.

KATIBU wa Idara ya Oganaizesheni ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Issa Gavu ametoa wito kwa viongozi wa serikali waliopewa dhamana ya uongozi kuhakikisha wanawatumikia wananchi wa nyanja zote bila kuwabagua.

Gavu ameto wito huo leo wakati wakati wa kongamano la kuliombea taifa ambalo limeandaliwa na Kanisa la Ufunuo lililopo Ubungo mkoani Dar es Salaam.

Amewahakikishia Watanzania kwamba wataendelea kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuwakumbusha na kuwasimamia viongozi wote wa serikali na kila aliyepewa dhamana kuhakikisha anatimiza wajibu wake ipasavyo.

"Dhamana waliyopewa viongozi wetu wa serikali ni ya kuwatumikia Watanzania walio wote bila kujali dini, rangi, makabila na wala jinsia zao,” amesema Gavu.

Pia amesisitiza kuwa viongozi wa dini ni watu muhimu sana kwa kuwa wamekuwa wakiliombea taifa pasipo wengine kufahamu, huku akiwaomba kuendelea kufanya hivyo kwaajili ya kupata ustahimilivu wa kitaifa.

"Lakini katika kila jambo unaloliona duniani wapo viongozi wanaochukua jukumu kwa niaba ya wengine kwenye hili jukumu la kumuomba na kumlilia Mungu niwaombe viongozi wetu wa kiroho msichoke endeleeni kuliombea Taifa,” amesema Gavu.

“Maombi yenu Mungu akiyapokea ndio baraka na neema kwa taifa lenu na viongozi wetu wa kisiasa na serikali msichoke kutukumbusha pale ambako panaondoka amani, upendo, na utulivu kwasababu endapo hayo yatatoweka, hata shughuli za ibada hazitapata nafasi ya kuwapa watu muda wa kuabudu kwa utulivu," amesema Gavu.

Kongamano hilo ni la kuliombea taifa litafanyika kwa siku tano ambako waumini zaidi ya 3,000 wanakutana kuliombea taifa.