DC Magoti ahimiza uadilifu mradi ujenzi wa kiwanda cha korosho

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 05:44 PM Oct 18 2024
Hafla fupi ya utiaji wa saini kati ya halmashauri ya wilaya hiyo na Mkandarasi Mohamed Builders LTD anayejenga kiwanda cha korosho.
Picha:Mpigapicha Wetu
Hafla fupi ya utiaji wa saini kati ya halmashauri ya wilaya hiyo na Mkandarasi Mohamed Builders LTD anayejenga kiwanda cha korosho.

MKUU wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti amesema ataendeleza kusimamia uadilifu kwa watumishi wa Serikali ili fedha zinazotolewa na serikali ziweze kutumika kama ilivyokusudiwa.

Magoti ameyasema hayo wakati wa hafla fupi ya utiaji wa saini kati ya halmashauri ya wilaya hiyo na Mkandarasi Mohamed Builders LTD anayejenga kiwanda cha korosho kwa gharama ya zaidi ya sh. bil. 2.55.

Akizungumza katika hafla hiyo alisema watumishi wanatakiwa kusimamia fedha zinazotolewa kwa uadilifu ziweze kuteleza miradi  kwa ufanisi kulingana na fedha zilizotolewa.

Kadhalika Magoti alimuomba mkandarasi huyo pamoja na kusaini mkataba wa mwaka mmoja ahakikishe anakamilisha ujenzi kabla ya muda huo Ili msimu ujao wa korosho wakulima wanufaike na kiwanda hiko.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Beatrice Dominic alisema fedha za mradi huo zilipitishwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 ikatangazwa kazi ambapo mkandarasi alipokea fedha ya awali sh. mil.438.

Dominic alisema mkandarasi aliingia kazini lakini michoro ilikuwa haijakamilika na  hivyo kusimamisha ujenzi hadi mwaka huu ambapo mkataba kwa mara nyingine umesainiwa kuanza kazi rasmi.

Aliwaomba wananchi kuachana na taarifa za mitandaoni ambazo hazina afya na kwamba mradi huo ambao ni muhimu kwa wananchi unaenda kuanza kazi na kuwa muarobaini kwa wakulima wa korosho kubanguliwa korosho zao ndani ya Wilaya ya Kisarawe.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Zuberi Kizwezwe aliomba wananchi kuendelea kuoamini Serikali kwenye fedha zinazotolewa kutekeleza miradi kwamba hakuna ifakayotumika kinyume na malengo.

Naye Khalfani Sika Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kisarawe alisema ujenzi wa kiwanda hicho unaenda kuwakomboa wakulima wakoroaho hivyo hatarajii kusikia Kuna kisingizio Cha kusua sua kwa mradi huo.

Mtaalamu mshauri ambaye ni msimamizi wa mradi huo Felician Mushi atahakikisha mradi huo unakamilika kwa muda uliotengwa  huku akisisitiza kutoa ushauri pale itakapohitajika