3061 Wahitimu SUA idadi ya Wanawake yaongezeka

By Christina Haule , Nipashe
Published at 08:12 PM Oct 18 2024
3061 Wahitimu SUA idadi ya Wanawake yaongezeka
Picha:Mpigapicha Wetu
3061 Wahitimu SUA idadi ya Wanawake yaongezeka

JUMLA ya wanafunzi 3061 wamehitimu masomo yao katika ngazi ya Shahada, Stashahada na Astashahada katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) huku idadi ya wanawake ikiendelea kuongezeka kwa kuwa wanafunzi 1,411 sawa na asilimia 46 ya wahitimu na wanaume wakiwa ni 1,650 sawa na asilimia 54.

Akitoa takwimu hizo katika Mahafali ya 44 ya Chuo hicho Makamu wa Mkuu wa Chuo Prof. Rafael Chibunda amesema wahitimu wa Shahada za awali wapo 2,809 ambapo kati yao wanaume 1,500, Shahada za Umahiri wahitimu 62, Stashada ya Juu ya Elimu wahitimu 3, na wahitimu wa Shahada ya Uzamivu 25.

Prof. Chibunda amesema wapo wahitimu 120 wa Stashahada na wahimu 42 wa Astashahada ambapo amewapongeza wahitimu hao na hasa wanawake kwa kufikia hatua hiyo .

Amesema SUA inastahili kujipongeza kwa mafanikio yanayooendelea kupatikana kila mwaka kwa kuongeza idadi ya nguvukazi yenye taaluma, ujuzi na weledi ambayo ni chachu ya kuongeza maendeleo katika nchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman amesema Baraza hilo limeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuboresha mafunzo kwa vitendo na kuongeza ujuzi wa wahitimu.

Aidha amesema Baraza linahimiza Menejimenti ya Chuo katika kutilia mkazo zaidi mafunzo kwa vitendo, kuboresha Mashamba darasa, Karakana za Uhandisi, Maabara na Misitu ya Mafunzo ili kutoa fursa kwa wanafunzi na wadau wengine wa kilimo kujifunza kwa vitendo ili kuongeza maarifa, ujuzi na umahili kwa wahusika.