Bilioni 977 zatumika Mradi wa EACOP, zaidi ya Watanzania 500 wapata ajira

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 08:25 PM Oct 18 2024
Mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi TPDC Balozi mstafu Peter Kallaghe akizungumza na vyombo vya habari muda mfupi baada ya kukagua mradi wa bomba la mafuta ghafi kata ya Igusule mkoani Tabora.
PICHA; SHABAN NJIA.
Mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi TPDC Balozi mstafu Peter Kallaghe akizungumza na vyombo vya habari muda mfupi baada ya kukagua mradi wa bomba la mafuta ghafi kata ya Igusule mkoani Tabora.

Mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongeleani, Tanga unavyoendelea na utekelezaji wake, tayari umegharimu kiasi cha Shilingi bilioni 977.

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi (EACOP), Asiad Mrutu, alipokuwa akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Ufundi inayosimamia madeni pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), iliyofanyika kijijini Sojo, Kata ya Igusule, Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora.

Mafanikio ya Mradi Mpaka Sasa

Mrutu amefafanua kuwa, mradi huo tayari umewaajiri zaidi ya Watanzania 500, huku ukisonga mbele kwa mafanikio makubwa. Kwa mujibu wake, hadi sasa jumla ya kilomita 1,004 za mabomba kati ya kilomita 1,443 zinazohitajika tayari zimewasili nchini, huku utekelezaji wa mradi huo ukiendelea kwa kasi na matarajio kuwa utakamilika ifikapo mwaka 2026.

Hakuna Ukosefu wa Fedha

Pamoja na changamoto mbalimbali zinazoweza kuibuka kwenye miradi mikubwa kama huu, Mrutu ameeleza kuwa hakuna tatizo la ukosefu wa fedha katika utekelezaji wake. Mpaka sasa, kiasi kikubwa cha fedha kimeshatumika, na hatua muhimu zimefikiwa. Ameongeza kuwa mradi huo uko ndani ya muda uliopangwa na hakuna dalili ya kucheleweshwa.

Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi (EACOP), Asiad Mrutu.
Ufidiaji wa Wananchi Umefikia Hatua Nzuri

Kwa upande wa wananchi ambao maeneo yao yalipitiwa na mradi huo, Mrutu ameeleza kuwa jumla ya wananchi 9,927 walipitiwa na wote wamefidiwa. Kati yao, 9,858 tayari wamepokea fedha zao, huku wengine wakipatiwa makazi ya kudumu. Hata hivyo, bado kuna wananchi 69 ambao fidia yao haijakamilika kutokana na masuala ya mirathi, lakini fedha zao zipo tayari kusubiri kukamilishwa kwa taratibu hizo.

Bodi ya TPDC Yarithika na Utekelezaji wa Mradi

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, Balozi mstaafu Peter Kallaghe, amesema bodi imeridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo. Kallaghe ameongeza kuwa, kiwanda cha kuweka koti la joto kwenye mabomba kilichopo Sojo kinaendelea na kazi kama ilivyopangwa, na wanatarajia mradi huo utakamilika kwa wakati.

Mradi wa EACOP unatarajiwa kuwa na athari kubwa kiuchumi, si tu kwa Tanzania bali kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki, kwa kuwa utafungua milango kwa biashara na ajira nyingi zaidi zinazoendana na sekta ya nishati na miundombinu.

Matarajio ni kwamba ifikapo mwaka 2026, bomba hilo litakuwa limekamilika na kuanza kufanya kazi, hivyo kuimarisha uchumi wa Tanzania na nchi za jirani kwa ujumla.