Kamishna Awadhi: Hatubebi chama,wanasiasa wamjibu "uhalisia una shida..."

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 01:49 PM Oct 18 2024
Kamishna Awadhi: Hatubebi chama,wanasiasa wamjibu "uhalisia una shida..."
Picha: Mpigapicha Wetu
Kamishna Awadhi: Hatubebi chama,wanasiasa wamjibu "uhalisia una shida..."

JESHI La Polisi nchini limewataka wananchi na vyama vya siasa kuacha kulinyooshea vidole kwamba linakandamiza baadhi ya vyama katika mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Uongozi wake umesema jeshi haliko kumlinda mtu au chama chochote kitakachovunja sheria na kuahidi kusimamia kutenda haki na si kuvunja haki.

Jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo, Kamishna Awadhi Juma Haji alitoa kauli hiyo kwa niaba ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) wakati wa mafunzo ya siku mbili (kuanzia jana) yaliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kuwajengea uwezo makamanda wa polisi mikoa kuelekea uchaguzi ujao.

Kamishna Awadhi ametoa kauli hiyo kipindi ambacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinamtuhumu kukiuka sheria za uchaguzi, pia yeye binafsi kuwapiga baadhi ya viongozi wa chama hicho, wakiwamo Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu na Katibu Mkuu John Mnyika. Kuna kusudio la chama hicho kumfungulia mashtaka mahakamani.  

Kamishna Haji aliwaomba Watanzania kuondoa dhana hiyo aliyoiita "potofu" kwa kuwa jeshi lipo kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa raia na kumwajibisha yeyote atakayekiuka sheria bila kujali ukubwa wa chama anachotoka.

"Hatupendelei mtu yeyote wala chama chochote kile, tuko katika majukumu mazito ya kusimamia sheria, hivyo kwa yeyote atakayekiuka sheria, basi tutawajibika, haijalishi ni nani," alisema.

Kamishna Awadhi alisema mafunzo hayo yamewakumbusha majukumu yao kwa kuwakumbusha kutoingilia kazi za watu wengine kama mahakama na taasisi zingine ambazo wanashabihiana katika utendaji kazi.

"Wajibu wetu mkubwa ni kuhakikisha tunadumisha amani katika kipindi hiki cha uchaguzi, kudumisha amani na haki ili Tanzania iendelee kuwa kinara wa amani katika demokrasia duniani kote," Kamishna Awadhi alisema.

Mratibu Kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa alisema wamewaleta pamoja makamanda hao ili kuwakumbusha kazi zao kuelekea uchaguzi kwa kusimamia sheria za uchaguzi.

"Pia kuwakumbusha maadili, miiko, misingi ya haki za binadamu wakati wa uchaguzi, mambo ya msingi wakati wa uchaguzi, uhuru wa kuongea, mbinu ambazo ni salama kutumia kulinda na kuleta amani wakati wa uchaguzi pasipo kumdhuru mtu yeyote," alisema.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, aliambia Nipashe jana kuwa wana imani na polisi, lakini watawapima zaidi kwa matendo yao kuliko maneno huku akiwataka kuacha kujivika alichodai "u-CCM" wanapotekeleza majukumu.

"Sisi tutawahukumu kwa matendo yao, tuna malalamiko mengi kwamba polisi wanasisima na CCM, hawatendi haki, wanawalinda watu wa CCM, tutawahukumu kutokana na matendo yao, popote watakapokwenda kinyume cha haki tutawasema," alisema.

Dorothy alisema ili anachokisema Kamishna Awadhi kiaminike, ni vyema wakaacha kuegemea chama kimoja, akitolea mfano wanavyozuiwa kufanya mikutano ya hadhara na baadhi ya viongozi kukamatwa saa chache kabla ya mkutano.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, alisema jana kuwa hakuna dhana kuwa polisi wanabeba chama kimoja bali kuna ushahidi wa wazi.

"Mpaka leo kijana wa CCM aliyemjeruhi kiongozi wetu kituoni Kata ya Tabata, Kituo cha Mtaa wa Msimbazi hajafikishwa mahakamani pamoja na kumjeruhi vibaya kwa kiwembe,  jambo ambalo lingeweza kusababisha kupoteza maisha.

"Tukio la pili lilitokea huko Ukonga, kijana wa CCM amemjeruhi vibaya kiongozi wa CHADEMA kwa kumpiga na jiwe. OCD wa Mpanda alizuia mikutano ya hadhara ya CHADEMA na kusema muda wa kampeni bado, ila vyama vingine vinaendelea na mikutano ya hadhara, huo ni ubaguzi na upendeleo wenyewe.

"Jeshi la Polisi litimize wajibu wake kwa mujibu wa sheria bila upendeleo wowote na watende haki kwa vyama vyote, wakifanya hivyo hapatakuwa na malalamiko," alisisitiza Mrema.