Ngorongoro mechi muhimu CAF

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 11:56 AM Oct 18 2024
Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Boniface Mkwasa.
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Boniface Mkwasa.

TIMU ya Soka ya Taifa ya vijana wa umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes), inatarajia kuwakaribisha Uganda katika mechi ya hatua ya nusu fainali ya michuano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA U-20), itakayochezwa leo kuanzia saa 9:00 mchana kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Mechi nyingine ya hatua hiyo inatarajiwa kuwakutanisha Kenya dhidi ya Burundi, itachezwa muda kama huo kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Timu mbili zitakazofanya vyema zitapata tiketi ya kuiwakilisha CECAFA katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U-20), zitakazofanyika baadaye mwakani.

Akizungumza na gazeti hili, Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Boniface Mkwasa, alisema wachezaji wake wameimarika na wamekuwa wakionyesha kiwango kizuri kadri mashindano hayo yanavyoendelea.

Mkwasa alisema anaamini watapata matokeo mazuri katika mechi hiyo na malengo yao makubwa ni kubeba ubingwa wa michuano hiyo mwaka huu.

"Mimi ni mzoefu na mashindano haya, timu inaweza kuanza vibaya, lakini uko mbele ikabadilika na hiki ndio kinaonekana, nawapongeza vijana kwa kuendelea kupambana. Kwetu kila mchezo ni muhimu na wao wanazidi kuzoea mashindano," alisema Mkwasa.

Aliongeza anafahamu Uganda wana kikosi kizuri na wataingia uwanjani kwa  kuwaheshimu.

"Uganda ni moja kati ya timu yenye wachezaji wazuri, wenye nguvu na vipaji vya kucheza soka, tuko tayari kwa mchezo huu, tunawaheshimu Uganda, lakini lengo letu lazima litimie, tukishinda kesho (leo), tutakuwa tumefuzu AFCON, lakini bado tunahitaji pia ubingwa wa CECAFA," alisema kocha huyo.