Prof.Kindiki ateuliwa Naibu Rais Kenya

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 11:25 AM Oct 18 2024
Prof. Kithure Kindiki
Picha:Mtandao
Prof. Kithure Kindiki

RAIS William Ruto amemteua Prof. Kithure Kindiki kuchukua nafasi ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambaye ameondolewa katika nafasi hiyo kufuatia uamuzi uliofuata taratibu za kikatiba kuanzia katika Bunge la Kitaifa na kuitimishwa katika Bunge la Seneti usiku wa kuamkia leo Oktoba 18, 2024.

Taarifa ya uteuzi huo imetolewa mapema leo Oktoba 18, 2024 na Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetangula mbele ya bunge hilo lililoketi kwa mujibu wa katiba kupitisha jina la Naibu Rais kutoka kwa Rais wan chi hiyo.

 “Kwa mujibu wa masharti ya Kanuni ya Kudumu ya 42(1), naomba kuripoti Bungeni kwamba leo asubuhi nimepokea ujumbe kutoka kwa Rais kuhusu uteuzi wa Kithure Kindiki kushika nafasi hiyo ambayo imetokea katika Ofisi ya Naibu Waziri. Rais wa Jamhuri ya Kenya kufuatia kushtakiwa kwa aliyekuwa ofisini hapo awali," Wetangula amesema. 

Prof. Kindiki, ambaye kwa sasa anahudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa, atahitaji idhini kutoka katika Bunge la Kitaifa kabla ya kushika nafasi ya Naibu Rais. Bunge lazima lipigie kura uteuzi ndani ya siku 60 baada ya kupokea jina hilo. 

Baada ya kuidhinishwa, mteule atateuliwa rasmi na Rais kuwa naibu wake. Ingawa Katiba haijaweka wazi muda wa uteuzi huo lakini unatarajiwa kutokea mara baada ya kuidhinishwa na Bunge.

 PROF.KINDIKI NI NANI. 

Prof. Kithure Kindiki alizaliwa mwaka 1972 miaka 52 iliyopita katika Kijiji cha Irunduni, Kaunti ya Tharaka Nithi, alihudhuria Shule ya Msingi ya Irunduni, kisha Shule ya Lenana, kabla ya kupata shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi. 

Baadaye alipata Shahada ya Uzamili na Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria. Aliporejea katika taaluma, alifundisha sheria katika vyuo vikuu vya Moi na Nairobi na mhadhiri katika baadhi ya vyuo vya nje ya nchi.

 Kindiki aliingia katika utumishi wa umma 2008 alipoteuliwa kuwa Katibu wa Uwiano wa Kitaifa na Maridhiano na marehemu Rais Mwai Kibaki. Alijiuzulu baada ya miezi mitatu, akitaja ukosefu wa nia ya kisiasa ya kuwapa makazi waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007. 

Kadhalika Kindiki alipata umaarufu nchini humo baada ya Ruto kumteua katika timu yake ya wanasheria wakati wa kesi ya uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Wakati huo Kindiki alirejea katika siasa, na kufanikiwa kuwania kiti cha Seneti cha Tharaka Nithi mwaka 2013 chini ya chama cha TNA.

 Alichaguliwa kwa mara ya kwanza na kuhudumu mihula miwili, akipanda hadi nafasi ya Naibu Spika katika muhula wake wa pili. Hata hivyo, mvutano ulipozidi kukua kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais Ruto, Kindiki alikabiliwa na changamoto katika Seneti na hatimaye kuenguliwa.

 Tangu wakati huo amehudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa katika Baraza la Mawaziri la kwanza na lililoundwa upya la Rais Ruto.

 Bunge la Seneti lilipiga kura ya kumuondosha Naibu Rais Rigathi Gachagua kufuatia mchakato wa siku mbili uliohusisha ushahidi wa kina na masaa ya kuhojiwa.

 Gachagua ameondolewa baada ya Maseneta kuunga mkono sababu tano kati ya kumi na moja zilizowasilishwa kama ufunguo wake wa kumtimua kati ya hizo zikiwemo ukiukaji mkubwa wa Katiba.