Tujitahidi kuondokana na aibu hii

By Joseph kulangwa , Nipashe
Published at 11:19 AM Oct 18 2024
Tujitahidi kuondokana na aibu hii
Mchoraji:Msamba
Tujitahidi kuondokana na aibu hii

KUNA mwaka fulani walikuja nchini Wazungu wawili; mke na mume wametoka Ulaya. Tuliwashuhudia barabarani tena katikati ya mji wakiwa wote wamevalia sketi!

Tuliwashangaa sana hususan mwanamume ambaye kwetu haijazoeleka. Tuliendelea kuwaangalia kwa mshangao na bahati nzuri walikuwa wakifuatana na mwenyeji wao, Mswahili mwenzetu, ambaye hatukusita kumwuliza kulikoni mwanamume kuvaa sketi kama mwanamke!  

Akatujibu ni utamaduni wa kwao. Akasema kwao Scotland, Uingereza, uvaaji huo ni wa heshima sana, hivyo hawaoni tatizo, basi tukaelewa, lakini wakituacha na mshangao wetu, huku tukijisemea nyoyoni kuwa kumbe hata Wazungu ni hamnazo, iweje mwanamume kuvaa kama mwanamke! 

Kumbe nikaja kubaini pia, kuwa kuna wakati vijana wetu wa kitanzania, lakini kabila la wafugaji Wamasai, walipata kwenda Ulaya nako wakasababisha mshangao kama hawa Wazungu wa Scotland, kwani wao walivaa lubega! 

Hivyo, kumbe utamaduni hutofautiana, kile wewe ukionacho kinakufaa kwa wengine huzua mshangao, lakini ni kutokana na kwamba tuna imani tofauti na kama hazina madhara, basi hapana budi kuzizingatia ili mradi zina mustakabali mwema kwa jamii husika. 

Kwa kuwa utamaduni ni imani na mfumo wa maisha ya jamii, hapana budi kukubalika na kutumiwa na jamii yote na hivyo matendo yake hufanana bila kutia chumvi na kuharibu staha ya wengine katika jamii hiyo husika.

 Hivi karibuni, nilikuwa nikitazama mtandaoni, ghafla nikamwona kijana mweusi akiwa nadhani Mmarekani, akijinasibu kukanyaga ardhi ya Marekani akitaka kila mtu ajue yuko huko. 

Kwa matendo yake, ilikuwa rahisi kila aliyemwona kuamini ilikuwa mara yake ya kwanza. 

Awali nilipoona majengo ya Marekani, haraka akili ikanijia kuwa pengine ni Marekani mweusi, kwani alikuwa katikati ya barabara akitamba na kushangilia, mara akirukia magari na kukumbatia watu. Lakini niliposikia 

lugha ya Kiswahili anaizungumza kwa ufasaha, nikadhani anatoka Mombasa. Nilipomwonyesha mwenzangu niliyekuwa naye jirani, akasema lafudhi ile ni ya kitanzania na si ya kimombasa. Hivyo nikaamini ametoka Tanzania. 

Swali nililobaki nalo kichwani, ni la kwa nini alikuwa akishangilia vile, mara akigalagala barabarani huku Wazungu wakimshangaa na wengine kumpisha. 

Akitembea katikati ya barabara kama aliye na changamoto ya afya ya akili, huku magari yakisimama na watu kumshangaa kapatwa na nini kijana yule, akirekodiwa na akimwelekeza mpiga picha wake amfuate kila anakokwenda akiendelea na tambo zake barabarani. 

Bila shaka wapita njia waliamini lazima kuna nati ililegea katika sehemu ya kichwa na ndiyo ikimfanya kupagawa vile, huku akijiita sijui balozi wa nini vile, akawa hasikiki vizuri bali makelele na kukumbatia watu akiwaambia: “Umepowaaa! Umepowaaa!” 

Jirani yangu akifuatilia kimya kimya picha ile jongefu, ghafla akavunja ukimya na kuniambia “achana na hao machawa tu, hawana lolote, angalia video zingine zenye akili kuliko hao”.  

Akiniambia siku hizi imekuwa kawaida watu kujifanya hamnazo, ili kupata wafuasi wengi kwenye mitandao.Akasema wengine wanajiita sijui mabalozi wa ‘Kazim bey’, sijui ndiyo nini, 

ila kwa kuwa sikutaka anione mshamba, nami nikanyamaza na kujifanya hata hiyo Kazim Bey naijua, lakini kumbe mbumbumbu tu mimi.  

Akaniambia wanatumiwa sana na wanasiasa siku hizi, na hivi tunakaribia uchaguzi ndiyo itakuwa balaa. 

Nikabaki najiuliza inakuwaje mtu atoke zake Tanzania aende nchi ya watu kufanya fujo barabarani akikumbatia watu asiowajua na kuwashika mikono bila kuelewa utamaduni wao ukoje?  

Nasema hivyo, kwa sababu nchi nyingi, mathalan za Mashariki ya Mbali huwa hawashikani mikono wala kukumbatiana wakisalimiana, bali huinamisha vichwa kuonyesha heshima tu. 

Sasa kama mtu utatoka huku na kwenda mahali usikojua utamaduni wao na kuwakumbatia eti “umepowaaa” huoni kama unasababisha sintofahamu? Ndiyo sababu katika picha ile jongefu, kijana yule wa kitanzania anakimbiwa au kupishwa na anaotaka kuwakumbatia au kuwashika mikono. 

Wahenga walishasema ukienda kwa wenye chongo, nawe vunja lako jicho, ili ufanane nao na ufuate utamaduni wao, kuliko kuwakera na ukichaa wako barabarani na kusababisha taharuki isiyo na lazima.  

Kwa maana nyingine starehe zako zisiwe kero kwa wengine. Hata kama tunatafuta wafuasi mitandaoni, basi tufanye kwa kiasi kuliko kuaibisha Taifa letu kwa sifa zisizo na kichwa wala miguu.  

Halafu inashangaza awamu hii ndiyo wameibuka machawa wengi wa aina hii wanaotuchefua kwa sifa rahisi rahisi! Tujirudi inawezekana, kwani muda upo bado.