MIAKA 18 YA MAADHIMSHO Siku ya Wanawake Waishio Vijijini na mzigo utamaduni unaowaelemea

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:22 AM Oct 18 2024
 

Mama wa kijijini akipambana na maisha.
PICHA: MTANDAO
Mama wa kijijini akipambana na maisha.

JUMANNE wiki hii Oktoba 15, dunia imeadhimisha Siku ya Wanawake Waishio Vijijini, huku ikielezwa kundi hilo linakabiliwa na changamoto lukuki, ikiwamo ukosefu wa elimu, ardhi, fursa za maendeleo, sambamba na kuathiriwa na mila kandamizi.

Wanawake kutoka maeneo tofauti ya vijijini nchini, wanaeleza changamoto wanazopitia kutokana na mazingira yao, akiwamo Aneth Mwinama, mkazi wa Kijiji cha Chikunja, Wilaya ya Masasi, Mtwara, anasema mifumo ya utoaji mikopo kwao walio vijijini haiendani na mazingira yao, hivyo inawanyima fursa.

"Kwa huku vijijini, wengi hatuchukui mikopo kwa sababu tuna kipindi cha kupata hela za mikopo, kwa kipindi cha kufikia Januari hadi mwezi wa Tano. Sisi wa vijijini hali zetu zinakuwa ngumu na biashara inakuwa ngumu. 

“Kuanzia mwezi wa sita hadi 12, wengi wetu tunakuwa na hali nzuri, kwa sababu pale tunauza mazao kama mbaazi na ufuta. Biashara zinakuwa zimechangamka," anaeleza Aneth.

Mwaka huu, siku hiyo imepambwa na kaulimbiu: "Wanawake wa vijijini wanaodumisha uoto wa asili, kwa mustakabali wetu wa pamoja, ili kujenga ustahimilivu wa mazingira, kuhifadhi baioanuwai na kutunza ardhi kuelekea usawa wa kijinsia na uwezeshaji."

JAMII YA KIHADZABE

Katika ufafanuzi wao, kuna maelezo yake Kilimba Kimatingu, Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira, anayefanya kazi kwa karibu na jamii ya Wahadzabe, wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha anao ufafanuzi.

Kilimba anasema wanawake wa jamii hiyo wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ardhi.

"Wanawake hawa wa Kihadzabe wamekuwa wakipata changamoto ya maeneo yao ya makazi kuuzwa na wanaume wa Kihadzabe. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha uliopita, 2022/2023, kulikuwa na ardhi ya makazi iliyouzwa kwa makabila mengine," anasema Kilimba.

Pia, anaeleza kinamama hao kutokana na mila zao, wanaamini katika kujifungua nyumbani, hali inayochagiza ukosefu wa huduma bora za afya ya uzazi kwa wanawake wa jamii hiyo. 

Mkazi wa Kata ya Domanga, Regina Biyo, naye anaeleza changamoto zinazowakabili wanawake katika maeneo yao.

"Kwenye tamaduni zetu, mama ndiye anajenga nyumba, mwanaume hahusiki katika hilo. Kwa hiyo, unakuta kwa asilimia kubwa mama ndiye ahangaike ajenge nyumba, watoto wale wavae, wafanyaje. 

“Haya ndiyo maisha yetu, hatulimi, tunategemea matunda na kuchimba mizizi ili watu wale. Inakuwa ngumu, ndiyo maana unakuta mama wa Kihadzabe anazeeka haraka kuliko wanaume."

MAADHIMISHO YALIKOANZIA

Siku ya Wanawake Waishio Vijijini ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mwaka 2007 chini ya Azimio mambari 62, ili kusherehekea umuhimu wa kundi hilo na kutumia muda huu kutafakari changamoto zao na kuzifanyia kazi.

Wanawake waishio vijijini, wanatajwa kuwa ndiyo uti wa mgongo wa mazao ya kilimo, wakichangia uzalishaji wa chakula na lishe na ndilo kundi linalosimamia ulinzi na usalama wa watoto. 

Hata hivyo, licha ya mchango wao, wanawake hao wanakabiliwa na changamoto lukuki hasa ukosefu wa haki ya kutoa maamuzi.

Siku ya Wanawake wa Vijijini, inatoa fursa ya kutambua na kusherehekea mchango wa wanawake hawa katika jamii, ikitajwa ni muhimu kuwapa wanawake wa vijijini fursa za elimu, rasilimali na uongozi ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii zao.

Hiyo itachangia si tu katika kuboresha hali zao, bali pia katika kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla. 

Kwa hivyo, inasisitizwa ni wajibu wa kila mmoja kuunga mkono juhudi za kuhakikisha wanawake wa vijijini wanapata haki na fursa zinazostahili.

 

·                 Kwa mujibu wa DW