Singida yawapeleka Yanga, Coastal Union New Amaan

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:50 AM Oct 18 2024
Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza.
Picha: Mtandao
Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza.

KLABU ya Singida Black Stars imetangaza rasmi mechi yake ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga itachezwa Oktoba 30, mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Sababu kuu ya kuupeleka mchezo huo Zanzibar ni mabadiliko yaliyofanywa na Bodi ya Ligi Kuu lakini pia kupisha ukarabati wa Uwanja wa Liti.

Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza, alisema sababu hizo mbili zimepelekea mabosi wa klabu hiyo kufanya uamuzi huo.

"Mnakumbuka Bodi ya Ligi imetangaza  mabadiliko ya ratiba, mchezo wetu dhidi ya Yanga awali hakukuwa umepangiwa tarehe ingawa ulikuwapo kwenye ratiba, kwa sasa umepangwa kuchezwa Oktoba 30, mechi yetu dhidi ya Azam, iliyopaswa tucheze Novemba 3, imerudishwa hadi tarehe 27, mwezi huo.

Vile vile mchezo wetu dhidi ya Coastal Union ambao katika ratiba ya awali ulikuwa uchezwe Novemba 7, mwaka huu umerudishwa nyuma hadi Novemba 2, tuna michezo mingine ya nyumbani dhidi ya Namungo na Fountain Gate, sasa kuna mabadiliko ya viwanja kwa sababu zote hizo hatutacheza kwenye uwanja wetu wa nyumbani," alisema Massanza.

Aliongeza tayari Bodi ya Ligi imetangaza kutoridhishwa na baadhi ya hali ya viwanja, hivyo michezo yao miwili dhidi ya Yanga na Coastal Union wataicheza kwenye Uwanja wa New Amaan ili kutoa muda wa kuukarabati uwanja wao wa Liti.

"Sisi tuna uzoefu, ukishaanza kuona hivyo ujue kuna dalili za kufungiwa uwanja, halafu tutaanza kutangatanga kutafuta viwanja vingine, kutokana na hilo tulikaa kama uongozi wa klabu katika vikao vya ndani, akiwamo meneja wa uwanja, akatuambia mechi nne zote zisichezwe kwenye uwanja huu utafungiwa," Massanza alisema.

Kutokana na tahadhari hiyo, mechi mbili tu kati ya nne watacheza kwenye uwanja huo, ambapo itacheza dhidi ya Namungo na Fountain Gate huku ile ya Yanga na Coastal Union wataipeleka kwenye Uwanja wa Amaan.