TRA yataja sababu madeni makubwa wafanyabiashara

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 02:16 PM Oct 18 2024
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda.
Picha:Mtandao
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda.

KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, amesema moja ya sababu za baadhi ya wafanyabiashara kuwa na madeni makubwa ya kodi kipindi cha nyuma ni kutokana na kutofautiana kwa rekodi.

Amesema kutokana na changamoto hiyo, kuanzia Januari, mwakani, serikali itaanzisha mpango wa kuwekeza katika Mfumo wa Kodi za Ndani (IDRAS) ambao utasaidia kuondoa changamoto hiyo na zile za migogoro ya kikodi na kurahisisha ukusanyaji. 

Mwenda aliyasema hayo jana katika kikao maalumu kilichoandaliwa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kujadili namna bora ya kukusanya kodi na kuondoa vikwazo katika taasisi za kifedha. 

Alisema lengo la kikao hicho ni kujadili namna ya kukuza biashara kwa taasisi za kifedha na kurahisisha upatikanaji wa kodi ambayo ndio msingi wa maendeleo ya nchi.

Mwenda alisema hatua ya mwisho kwa watakaokuwa wakaidi kulipa kodi watatumia mawakala wa benki japo zipo njia ambazo watazitumia awali kabla ya kufikia hatua hiyo. 

“Kwanza hatuwezi kutumia wakala wa benki bila kumpeleka mlipakodi ‘demand note’ (taarifa kwa mhusika kumhitaji alipe) lakini pia hatuwezi kufanya hivyo bila kupeleka ‘reminder note’ (taarifa ya kumkumbusha). 

 Hapo lazima tuwaite tukae nao tuwasikilize na tuwape fursa ya kulipa kidogo kidogo.  Lazima tuwaandikie barua ya nia ya kutumia benki kama mawakala lakini njia hiyo haiwezi kutumika mpaka mimi nijiridhishe,” alifafanua. 

Hata hivyo, alisisitiza hatamani kufikia katika hatua hiyo kwa kuwa njia hizo ni ndefu na kwamba atahakikisha wanatumia njia nyingine kufikia suluhu. 

“Tutakaa nao tutajenga uhusiano ili tukubaliane namna bora ya wao kulipa madeni na kuwashauri waendelee kutumia huduma za kibenki kwa kuwa itawaweka katika nafasi ya kupata mikopo mikubwa kwa ajili ya kuendesha biashara zao. 

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, alisema majadiliano hayo ni ya kuangalia namna ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwezesha taasisi za kifedha kusaidia shughuli za kibiashara ili kuongeza ukusanyaji wa kodi.  

Alisema benki ni miongoni mwa taasisi zinazolipa kodi kubwa na inatumika kama mawakala wa kukusanya kodi na kutunza fedha za walipakodi na kwamba kutokana na umuhimu huo kuna haja ya kuwa kitu kimoja ili kuboresha mazingira hayo. 

Akizungumza kwa niaba ya benki zingine na taasisi za kifedha, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Theobald Sabi, alisema wamefurahi kukutanishwa na TRA na BoT kujadili masuala ya kodi na kufahamishwa hatua zilizochukuliwa. 

Sabi alisema hatua hizo zitawapa wateja wao morali ya kuendelea kutumia kuweka fedha benki huku akisifu zitaleta matokeo chanya na kuwapa wateja imani kubwa ya kutumia mifumo rasmi katika biashara.