Bacca ashusha presha Yanga

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:44 AM Oct 18 2024
 Ibrahim Abdallah 'Bacca'
Picha: Mtandao
Ibrahim Abdallah 'Bacca'

HALI ya beki wa kati wa Yanga, Ibrahim Abdallah 'Bacca' ni nzuri na mlinzi huyo atacheza mechi dhidi ya watani zao, Simba itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, imeelezwa.

Yanga imelazimika kutoa kauli hiyo kufuatia tetesi huenda Bacca akaukosa mchezo huo kwa sababu ni majeruhi.

Sintofahamu hiyo imeenea baada ya beki huyo kuweka picha ya kupata jeraha kwenye kifundo chake cha mguu baada ya kumalizika kwa mechi kati ya Timu ya Taifa (Taifa Stars), dhidi ya DR Congo, iliyochezwa Jumanne hapa nchini.

Hata hivyo Bacca hakuandika maneno yoyote katika picha hiyo, ingawa baadhi ya  wachambuzi walidai Mzanzibar huyo aliumia katika mechi hiyo ambayo Stars ililala mabao 2-0.

Meneja wa Yanga, Walter Harrison, alisema jana mchezaji pekee ambaye ni majeruhi katika kikosi chao ni Farid Mussa lakini ameshaanza mazoezi maalum ya kurejesha utimamu wa mwili, kabla ya kujumuika pamoja na wenzake.

"Hakuna taarifa yoyote ya majeruhi, na wachezaji wote waliokuwa kwenye vikosi vya timu za taifa, wameshawasili, hakuna yoyote aliyerejea akiwa na majeraha, mtu pekee ambaye bado na matatizo ni Farid, na yeye pia ameshaanza mazoezi mepesi ili kurudisha utimamu wa mwili kabla ya kujiunga na wenzake.

Nasema hakuna taarifa yoyote nyingine ya upande wa majeraha ya wachezaji wetu, kikosi chetu kiko imara na tayari kwa dabi hiyo," Harrison alisema.

Kuhusu mchezo husika, meneja huyo alisema maandalizi yao yanaendelea vizuri kwa sababu walikigawa kikosi chao pande mbili.

"Kila kitu kinaenda vizuri, tumekuwa na timu mbili, iliyobaki Dar kambini, na ile ya wachezaji waliokuwa wamekwenda kuzitumikia timu zao za taifa, ni kama timu mbili tofauti.

Tulipata muda mzuri wa kujumuika na kikosi cha timu ya vijana wa umri chini ya miaka 20, tulifanya nao mazoezi na tulicheza michezo miwili dhidi yao, hivyo wachezaji waliobaki kambini walipata muda wa kutengeneza pumzi na utimamu wa mwili, benchi la ufundi lilipata nafasi kuona wamefikia wapi na kutengeneza uwiano ili wenzao watakaorudi kutoka timu za taifa wake tayari," meneja huyo aliongeza.

Alisema Yanga haina hofu yoyote kuelekea mechi hiyo na hawana maneno zaidi ya kuzungumza kwa sababu wanasubiri muda wa vitendo.

"Tupo kambini kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kila kitu kinaenda vizuri, kila mtu anajua nini anatakiwa kukifanya, nadhani nilishazungumza hapo awali, aina hii ya michezo si ile ambayo benchi la ufundi wanalazimika kuongea sana kwa sababu inajizungumza yenyewe kwa ukubwa wake," aliongeza kiongozi huyo.

Taarifa hiyo ya Harrison, imeleta faraja kwa wanachama na mashabiki wa Yanga, ambao waliingiwa na wasiwasi ya kumkosa beki huyo ambaye amekuwa  tegemeo kubwa katika eneo la ulinzi.

Kwa upande wa Simba, mashabiki wao walishaanza 'kuwakoga' wenzao wakitamba endapo beki huyo atakosekana, timu yao inajiandaa kupata idadi kubwa ya mabao kutokana na hali ya mastraika wao wanaoongozwa na Leonel Ateba.