Simba: Mashabiki wanatudai

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 11:39 AM Oct 18 2024
Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr'
Picha: Mtandao
Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr'

IKIWA imebaki siku moja kabla ya mchezo wa Dabi ya Kariakoo, baadhi ya wachezaji waandamizi wa Simba wamesema wanaona wanadeni kwa mashabiki wao hivyo lazima wapambane na kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Yanga hapo kesho.

Simba atakuwa mwenyeji katika mchezo huo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa mwaka 2024/2025.

Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara watashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi wa mechi zote mbili za msimu uliopita, lakini pia ikiwafunga Simba bao 1-0 kwenye mechi ya hatua ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii msimu huu.

Akizungumza na gazeti hili jana, nahodha wa Simba, Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' alisema wanafahamu umuhimu wa mchezo huo na mategemeo ya mashabiki wao.

Zimbwe alisema kwao wanaichukulia mechi hiyo ina umuhimu mkubwa 'sana' hasa baada ya kutofanya vizuri katika michezo mingine ya dabi waliyocheza hivi karibuni.

"Tunaendelea na maandalizi yetu vizuri, tunaahidi tutapambana ili kuhakikisha tunawalipa mashabiki wetu, upendo na hamasa yao wanayotupa sisi kwetu kama wachezaji ni sawa na deni," beki huyo wa zamani wa Kagera Sugar alisema.

Aliongeza matokeo ya mwisho ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union hayakuwa mazuri na kwao wanayachukua kama funzo kuelekea katika mchezo dhidi ya watani zao.

"Mashabiki waendelee kutusapoti, tutapambana kwa kila namna kuhakikisha tunapata ushindi, tunajua tuliwaumiza katika mechi ya mwisho kabla ya kwenda kwenye majukumu ya kimataifa," aliongeza beki huyo wa pembeni wa Timu ya Taifa (Taifa Stars).

Naye Shomari Kapombe, ambaye ni mchezaji mwandamizi wa timu hiyo iliyoko katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi alisema wachezaji wote wapo tayari kwa ajili ya kusaka ushindi kwenye mchezo huo wa kesho.

Beki huyo wa zamani wa Azam FC amewataka mashabiki na wanachama wa Simba kutokuwa na wasiwasi kwa sababu wamejipanga kuwalipa furaha.

"Benchi letu la ufundi linaendelea kufanya kazi yake na sisi wachezaji kazi yetu itaonekana uwanjani Jumamosi (kesho), naamini tutafanya vizuri, tunajua namna mashabiki wetu wanavyoisubiria hiyo mechi, huu ni msimu wao," Kapombe alisema.

Ubora na ushindani uliopo kwa wachezaji wa timu zote mbili unaufanya mchezo huo wa dabi kusubiriwa kwa hamu na idadi kubwa ya mashabiki kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Singida Black Stars yenye pointi 16 kibindoni, ikiwa imeshinda mitano na sare moja, ikifunga magoli tisa na kuruhusu nyavu zake kuguswa mara tatu, ndio vinara wa ligi hiyo wakifuatiwa na Simba yenye pointi 13, imecheza mechi tano.

Yanga ina pointi 12 na imeshuka dimbani mara nne tu, iko katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 kutoka mikoa mbalimbali.

Vigogo hao wawili wote wametinga hatua ya makundi ya mashindano ya kimataifa, Yanga ikipanga Kundi A kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Wekundu wa Msimbazi pia wakiwa Kundi A kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.