Madarasa shambani, mkakati shirikishi unavyotibu parachichi kumeaMufindi

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 11:14 AM Oct 18 2024
 Ofisa Kilimo Mwandamizi wa Wilaya ya Mufindi, Patrick Vavunge (mwenye fulana nyeusi kushoto) na wadau wa kilimo cha parachichi, kwenye shamba darasa lililoko wilayani Mufindi.
PICHA ZOTE: RENATHA MSUNGU
Ofisa Kilimo Mwandamizi wa Wilaya ya Mufindi, Patrick Vavunge (mwenye fulana nyeusi kushoto) na wadau wa kilimo cha parachichi, kwenye shamba darasa lililoko wilayani Mufindi.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mufindi sasa imejipanga kuhakikisha kilimo cha parachichi, kinazidi kukua kwa kasi zaidi.

Sasa imepanga ina orodha ya mikakati mbalimbali waliojiwekea kama halmashauri, ili kuwainua wakulima wa eneo hilo. 

Mojawapo ni kuhakikisha wanashirikiana na taasisi zisizo za kiserikali, ikiwamo Rural Development Organizatiom (RDO) na nyinginezo, kuhakikisha wakulima wanapata uelewa kwenye kilimo wanachokiendesha.

 Dira ya halmashauri hiyo ni kuwahakikisha wakulima wake wanaondoka katika kilimo cha mazoea kisichofuata kanuni za maofisa ugani katika maeneo yao, badala yake wahamie kutumia teknolojia.

 Mikakati hiyo, imeonyesha kusaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza mavuno ya wakulima wa vikundi, pia mmoja mmoja wanaozalisha parachichi.

 Patrick Vavunge, Ofisa Kilimo Mwandamizi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, anataja kuwa eneo la kilomita za mraba 6,170, sawa na hekta 617,000, huku kunakofaa kwa kilimo ni hekta 567,640.

 Vavunge anasema, parachichi inayolimwa kwa mwaka msimu wa kilimo 2023/2024 ni hekta 1,278, sawa na ekari 3,178,  kutoka kwa wakulima wa vikundi na mmoja mmoja wanaolima kibiashara. 

Anafafanua zaidi, wakulima parachichi waliotambuliwa na halmashauri hiyo ni 1,351 hadi Machi mwaka huu, kila mwaka wakiongezeka kwenye kilimo hicho. 

“Takwimu hizi zinaendelea kupanda mwaka hadi mwaka, kwa sababu wakulima wanazidi kuongezeka kwenye kilimo hicho ambacho hustawi kwa kiasi kikubwa katika halmashauri hiyo,” anasema Vavunge.

 Anafafanua kuwa, halmashauri Mufundi imekuwa ikiwafunza wakulima namna ya kufuata kanuni, wakishirikiana na taasisi binafsi ya Rural Development Organization (RDO) kuhakikisha kunakuwapo kilimo chenye tija.

 Anayataja, mafunzo hayo ni muhimu kutokana na uelimishaji wake kuhusu parachichi, zao wanalolitumia kwa biashara mkoani humo.

 Vavunge anasema, halmashauri hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu Bora Tanzania (TOSCI), inatoa mafunzo kwa wakulima na kampuni zinazozalisha mbegu, kuhakikisha wakulima wanatumia mbegu bora ya parachichi.

 KIWANGO MAVUNO 

 Kuhusu kanuni bora, Vavunge anasema wanaolima kienyeji huvuna kwenye mti mmoja kuanzia parachichi 100, lakini wanaofuata kanuni huvuna kati ya 150 hadi 180.

 Pia, anafafanua kwamba wanaotumia teknolojia, kwa mti mmoja huvuna kuanzia parachichi 200. Hiyo ni kutokana na eneo ambalo mkulima amelima. 

“Tunajitahidi kutoa elimu ili wakulima wote wafikie idadi ya mavuno ya parachichi 200 kwenye mti mmoja, lengo ni wazidi kuinuka kiuchumi kupitia zao hilo la parachichi,” anasema Vavunge.

 Anaelezea kuwa uzalishaji kwa mwaka huu umeongezeka, kutoka tani 618.5 za mwaka 2022/23 hadi tani 705 kwa mwaka 2023/2024, na hiyo imetokana na kuwatambua wazalishaji mbegu bora, wanaopata mafunzo kutoka TOSCI, kwa kushirikiana na taasisi nyinginezo. 

Anasema taasisi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo ya uzalishaji miche bora ya parachichi na mazao menginena wanawapatia vyeti baada ya kuhitimu na wanaendelea kutawanya michezo kwa wakulima.

 MDAU MWANDAMIZI

Mkurugenzi wa Asasi ya RDO, Fidelisi Filipatali, anasema mbali na madarasa ya parachichi, pia wanafunzi wakulima kwa kushirikiana na serikali, vijana wanapata  elimu kilimo kwa vitendo.

 Anataja fursa wanazotoa zinajumuisha mafunzo kwa vijana wanaochipukia kwenye kilimo, pia wanaungana na serikali kuwekeza kwenye mazao ya bustani. 

Filipatali anawataja washirika wao wakuu ni Halmashauri Wilaya ya Mufindi, hasa katika uzalishaji parachichi, vijana nao wakinufaika kupata mafunzo ya zao hilo. 

“Ardhi ya Mufindi inakubali mazao mbalimbali, ikiwamo zao hilo. Hivyo,wakulima wanapaswa kujitokeza kulima parachichi kwa sababu soko lake lipo na serikali inasaidia kuwatafutia wakulima masoko ya zao hilo,” anasema Filipatali. 

Anafafanua Mufindi na halmashauri nyinginezo mkoani Iringa, kunaonyesha ustawi unatokana na maofisa kilimo wake wanawatembelea wakulima na wanawapa elimu na maelekezo ya kitaalamu. 

Filipatili anafafanua, siri ya mafanikio katika zao hilo inatokana na wataalamu wa kilimo, wanaotoa maelekezo kwa wakulima kulima kilimo hicho cha biashara mkoani Iringa, lengo ni kukifanya kizoeleke katika ubora wa pekee. 

Anasema wanalima parachichi, kupitia maelekezo kutoka kwa wataalamu wanaotoka serikalini, ambao wanawatembelea wanakolima kuwapa elimu na kukagua maendeleo ya shambani. 

"Kilimo mkoani hapa kinastawi sana na hii inatokana na wakulima kulima kilimo cha kisasa kwa kufuata maelekezo kutoka kwa wataalam wa kilimo wa sekta hiyo," anasema Filipatali. 

WAKULIMA PARACHICHI 

Wakulima wa parachichi, wana maoni kwamba ni kilimo chenye tija, endapo mkulima atafuata kanuni zinazotolewa na wataalamu kabla ya kuanza kuotesha miche na msimu wa mavuno unapowadia.

 Josephat Mgimwa, anasema hivi sasa wakulima wengi wanafurahia matunda kujikita katika kilimo hicho, kutokana na kufuata kanuni zinazoelekezwa na maofisa ugani wao katika maeneo yao ya kilimo.

 Mgimwa anatoa mtazamo wake kwamba, kilimo hicho kinapoendeshwa kwa ufasaha, kinachangia kwa kiasi kikubwa kuwainua wakulima kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini, akisisitiza haja ya kuwekezwa zaidi, ili kuwainua wakulima. 

MAOFISA KILIMO  

Vavunge anasema, changamoto kubwa wanayokutana nayo inajumuisha baadhi ya wakulima wanashindwa kutofautisha magonjwa yanayolikabili zao la parachichi na kukosekana virutubisho lishe kwenye zao hilo.

 Anasema, imekuwa kawaida kumtembelea mkulima anayeelezea changamoto ya zao hilo shambani pale, katika ufafanuzi wake anapohojiwa anaangukia majibu ya kuwapo makosa katika uwekaji virutubisho vya zao wakati wa uoteshaji miche. 

Kutokana na hilo, anasema maofisa ugani wamekuwa wakiwaelekeza wakulima namna ya kuhudumia parachichi tangu awali, hadi ngazi ya mavuno. 

Rai yao sasa wataalamu wa kilimo kwa serikali, ni kwamba itoe mafunzo kwa maofisa ugani ya utunzaji vizuri wa zao la parachichi, kwa sababu katika miaka ya nyuma lilikuwa halilimwi.

 Anasema linakuwa zao geni, hata mafunzo kwa maofisa ugani yanatakiwa kila mara, ikiwamo kuhusu magonjwa ya parachichi, yanayopaswa kutolewa kwa maofisa ugani, nao wapeleke ujuzi wanaovuna mafunzoni kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini. 

Pia, anaiomba serikali kutoa vibali vya kuajiri maofisa ugani zaidi, kwa sababu waliopo ni wachache, akitumia mfano wachache wa Mufundi wanahudumia vijiji 121 na vitongoji 561. 

“Tunaishukuru serikali kwa kuajiri maofisa ugani, lakini tunaomba izidi kutoa vibali vya kuajiri kuongeza ufanisi wa kazi za kila siku kwenye sekta ya kilimo,” anasema Vavunge.

 Anafafanua kuwa, wataalamu wa mazao ya bustani wako wachache, nako serikali iongeze watu wa sekta hiyo, kukabiliana na changamoto zilizoko katika  mazao mbalimbali.

 MIKAKATI YA WATAALAMU 

Vavunge anataja mikakati waliojiweka Halmashauri ya Wilaya (Mufindi), inajumuisha kuwaunganisha wakulima kwenye vikundi na kuwatafutia soko, kwa bei elekezi kutoka vyama vya ushirika.

 Anataja mingine, ni kuwatambua wakulima parachichi waliopo kwenye vikundi, pia wanaolima kipekee, nao wawakaribishe katika soko la parachichi.

 Inatajwa, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, sasa ina mpango wa kujenga nyumba ya kuhifadhia zao hilo, kabla hayajapelekwa kwenye soko la nje.

 Vavunge anaishukuru serikali, kwa ushirikiano anayotaja wanaupata kwenye sekta ya kilimo, kitendo kinachochangia sekta hiyo izidi kukua mkoani Iringa.