Mkulima kuwaburuza kortini vigogo kwa tuhuma kushusha bei ya pamba

By Remmy Moka , Nipashe
Published at 02:42 PM Oct 18 2024
Pamba
Picha:Mtandao
Pamba

MKULIMA wa pamba, Thomas Nkola, mkazi wa mkoani Simiyu, ameeleza nia ya kuwashtaki baadhi ya wabunge na viongozi wa Bodi ya Pamba, akiwatuhumu kushusha bei ya pamba mkoani Simiyu na kuwasababishia hasara wakulima.

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Mwanza juzi, mkulima huyo alisema pamba ni uti wa mgongo kwa wakazi na wakulima wa Simuyu, lakini wakulima hao wamekuwa hawanufaiki na kilimo hicho kutokana na watu wachache, wakiwamo wabunge, kutajinufaisha nacho.

Nkola alisema yupo katika hatua za mwisho za kufungua kesi dhidi ya baadhi ya wabunge wa majimbo ya mkoa huo na jimbo moja la mkoani Tabora.

Alisema lengo la kuwaburuza vigogo hao ni kutokana na madai kwamba wameshindwa kuwajibika kwa nafasi zao kuhakikisha kunakuwa na ununuzi mzuri wa pamba, huku baadhi yao wakidaiwa kulazimisha kuwa wanunuzi wa zao hilo.

"Kesi hiyo itahusisha pia viongozi wa Bodi ya Pamba na wengine ambao wote hao wameingia katika bodi ya pamba kinyume cha utaratibu na kushusha bei yake kwa manufaa yao binafsi," alidai Nkola.

Alidai kuwa hivi sasa mfuko mmoja wa mbegu ya pamba unauzwa kwa Sh. 10,000 na viwatilifu kwa kila ekari moja vinagharimu Sh. 15,000, jambo linalosababisha wakulima kutofaidika na kilimo wakati wa mavuno.

Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Mkoa wa Simiyu, Robert Mafuru, alisema chama chao kinaungana na mkulima huyo kuhakikisha wakulima wa mkoa huo wanapata haki yao kupitia kilimo cha pamba.

Mafuru alisema falsafa ya chama hicho inahimiza maendeleo, hivyo hakuna budi kumuunga mkono mkulima huyo katika hatua zote za ufunguzi wa kesi na kuhakikisha wakulima wote wananufaika na pamba.

"Tupo tayari kumpatia wanasheria watakaosimamia kesi hiyo na kuhakikisha haki inapatikana kwa maslahi mapana ya wakulima wa zao la pamba mkoani  Simiyu," alisema Mafuru.