Vijiji 14 kuwekwa kwenye mipango ya matumizi ya ardhi Rombo

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 05:21 PM Oct 18 2024
Vijiji 14 kuwekwa kwenye mipango ya matumizi ya ardhi Rombo
Picha:Mpigapicha Wetu
Vijiji 14 kuwekwa kwenye mipango ya matumizi ya ardhi Rombo

TUME ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imesema inaandaa mipango ya matumizi ya Ardhi ya Vijiji 14 wilayani Rombo, Kilimanjaro lengo likiwa ni kuhakikisha kunakuwa na milki salama za ardhi.

Hayo yamebainishwa juzi na Ofisa Mipango Miji kutoka NLUPC, John Chuwa aliyeambatana na wataalam wengine wilayani Rombo kwaajili ya kuwezesha utekelezaji wa mpango huo.

Chuwa alisema kupitia mpango huyo Tume hiyo imeandika historia katika jitihada za kuisaidia halmashauri hiyo kuongeza uzalishaji wenye tija, uhifadhi wa mazingira pamoja na kuzuia migogoro ya ardhi.

Akizungumza na wataalamu hao, Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa aliahidi kutoa ushirikiano ili kuweza kufanikisha zoezi hilo la uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi katika Vijiji vilivyobainishwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Rombo ,Raymond Mwangwala alieleza kufurahishwa na ujio wa mpango huo na kuwa usaidia kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi na kuchochea maendeleo endelevu katika Vijiji na Wilaya hiyo.

Aidha katika hatua nyingine wataalamu kutoka Tume wakiongozwa na Chuwa ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo waliendesha mafunzo kwa Timu Shirikishi ya Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi ya Wilaya (PLUM).

Chuwa alisema timu hiyo inayoundwa na wataalamu kutoka sekta mbalimbali zinazohusika na matumizi ya ardhi katika Halmashauri hiyo.

"Mafunzo haya yamefanyika kwa mujibu wa Mwongozo wa Uandaaji na Usimamizi Shirikishi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji nchini ili kuwajengea uwezo wahusika kutoka timu ya PLUM kabla ya kuanza zoezi la Uandaaji wa Mpango wa matumizi ya Ardhi," alisema Chuwa.