Vijana 300 waungana kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi

By Allan Isack , Nipashe
Published at 05:52 PM Oct 18 2024
Vijana 300 waungana kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi
Picha: Mpigapicha Wetu
Vijana 300 waungana kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi

ZAIDI ya vijana 300 kutoka mataifa 100 Duniani wamekutana kwa siku tano katika Chuo cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataif (MS TCDC),kupitia kambi ya haki ya hali ya hewa wakijadiliana namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mratibu wa Kambi ya Haki ya Hali ya Hewa,Augustin Maggio,kutoka nchi ya Argentina,alisema hadi sasa kambi hiyo wameifanya kwa muda wa miaka mitatu ambapo kwa miaka miwili iliyopita walifanya katika eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.  

“Kambi ya uzinduzi ilifanyika katika nchi ya Tunisia, kisha ikafuata  huko Lebanon, ambako  mwaka jana iliwashirikisha vijana takribani 500” alisema Maggio. 

Hata hivyo,alisema wana uzoefu wa kufanya kambi hizo, kuendesha warsha na kutoa mafunzo kwa kuwa kumechangiwa waandaaji, wanaharakati na watetezi kutoka maeneo hayo, kwa ajili ya kubadilisha jamii zao. 

“Ujumbe pamoja na shuhuda tunazopata kwa vijana hawa kutoka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kuhusu ni kwa namna gani kambi hii inaweza kusaidia kwenye maeneo ya jamii zao,”aliongeza.

Na ni kwamba, tumekuwa tayari kwa muda mrefu kuleta jukwaa hili hapa. Tumekuwa tukifanya kazi na washirika wengi wa ndani, kutoka Kenya, kutoka Tanzania, kutoka Afrika Kusini, kutoka Uganda, na hatimaye tuliweza kuiweka pamoja. 

Aidha alisema kambi hiyo,imeunganishwa na zaidi ya mashirika 30 ya wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu, yakiwamo kutoka hapa nchini na nje ya nchi.

Naye Hapyness Njile,kutoka taasisi ya Agline Peace Afrika,alisema jukwaa hilo,limewakutanisha vijana kwa kuwa imeonekana wao ndio waathirika wakubwa wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

“Tumekutana hapa kuangalia ni namna gani tutakavyoweza kupambana na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa kundi la vijana wamekuwahanga kwa kuwa wana wajibika kwenye sekta zote ikiwamo kilimo na uchimbaji madini,”alisema.

Alisema katika jukwaa hilo,amejifunza namna ya kwenda kuelimisha jamii ikiwamo kutunza mazingira hasa kutokutupa taka ovyo na kukata miti kwa ajili ya shughuli za kibinadamu. 

Mdau wa mazingira ambaye ni,mshiriki katika kambi hiyo,kutoka taasisi ya Green Conserver,Ziada Kasimu,alisema wamekuwa wakishirika katika harakati za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,utunzaji wa mazingira pamoja na nishati mbadala. 

“Athari za mabadiliko ya tabianchi inaweza kuchangia kushuka kwa nchi kimaendeleo kwahiyo kinana anapaswa kuwa mstari wa mbele kupambana na athari hizo kwa kuwa ndio nguvu kazi tuliyonayo kwa sasa,”alisema.