Tatizo usafiri wa boti Mafia lichukuliwe kwa uzito mkubwa

Nipashe
Published at 01:30 PM Oct 18 2024
Tatizo usafiri wa boti Mafia lichukuliwe kwa uzito mkubwa
Picha:Mtandao
Tatizo usafiri wa boti Mafia lichukuliwe kwa uzito mkubwa

KUMEKUWAPO na taarifa kwamba wakazi wa kisiwa cha Mafia katika mkoa wa Pwani, wanalalamikia kukosekana kwa usafiri wa uhakika wa boti kwa takriban wiki mbili sasa.

Sababu kubwa ya kukosekana kwa usafiri huo unaotegemewa na wengi, kwa mujibu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), kivuko kilichokuwapo kupata hitilafu kwenye injini baada ya moja kufa na ikabaki moja inayofanya kazi, hivyo kusimama kutoa huduma. Kutokana na tatizo hilo, TEMESA imewaomba wananchi hao kuwa wavumilivu na kuacha kutumia usafiri usio salama kama wa kutumia mitumbwi. 

Kutokana na kukosekana kwa usafiri huo, wananchi wa kisiwa hicho wamejikuta wakilazimika kutumia mitumbwi kwenda katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutafuta mahitaji. Kwa mujibu wa wananchi hao, kwa kukosekana kwa boti inayotoka na kuingia kisiwani humo, wanatumia majahazi na boti za wavuvi kutokana na kushindwa kumudu gharama za usafiri wa ndege.

Aidha, sehemu inayofungua milango ya mawasiliano kati ya Mafia na maeneo mengine ni Nyamisati wilayani  ambako baada ya kufika wanaweza kusafiri kwa aina nyingine ya usafiri na hatimaye kupata mahitaji yao muhimu. Kutokana na kutokuwapo kwa boti hiyo, walisema wanasafiri hata kwa siku mbili hadi tatu kufika Nyamisati tofauti na saa nne hadi tano wanazotumia kukiwapo boti.

Tatizo hilo pia limesababisha hata wagonjwa wanaohitaji rufani kwenda Dar es Salaam au hospitali zingine kubwa kwa matibabu kuwa katika wakati mgumu hata hatari ya kupoteza maisha. Licha ya wagonjwa, pia wananchi wanashindwa kupata mahitaji muhimu ambayo mengi yanapatikana Dar es Salaam. 

Kwa jumla, wananchi wengi wa kisiwa cha Mafia ni wa kipato cha chini, hivyo unapokosekana usafiri wa meli au boti ya uhakika, wanakuwa wamefungwa. Hali hiyo ni kwa sababu wanaoweza kutumia usafiri wa anga, kwa maana ya ndege ni wachache. Kwa mantiki hiyo, kutokuwapo kwa usafiri wa majini kunawafanya wakose mahitaji muhimu, kama vile vyakula na vinywaji, ambayo mengi yanatoka maeneo ya nchi kavu kama Kibiti, Dar es Salaam na Mkuranga. 

TEMESA imetoa ufafanuzi kwamba kukosekana kwa usafiri huo kunatokana na kufa kwa injini moja kati ya mbili za boti hiyo, hivyo kulazimika kuipelekwa kwenye matengenezo. Sababu hiyo ni nzuri kwa usalama wa chombo hicho lakini haitoshi bali taasisi hiyo ilipaswa kuchukua hatua ili kuwa na usafiri wa muda wakati ule wa uhakika unapofanyiwa matengenezo. 

Kwa kuzingatia mazingira na umuhimu wa mahitaji ya wananchi wa kisiwa cha Mafia, serikali kupitia TEMESA ilipaswa kukodi boti ili kuwawezesha kupata usafiri badala ya kuwaacha wakiteseka kama ilivyo kwa zaidi ya wiki sasa. 

Hivi karibuni kulikuwa na shida ya usafiri wa boti kati ya Feri na Kigamboni mkoani Dar es Salaam lakini kutokana na mahitaji makubwa ya usafiri huo, serikali ilichukua hatua kwa kutumia boti za biashara kukwamua tatizo. Inakuwaje jambo kama hilo kushindikana kwa kisiwa cha Mafia ambacho usafiri mkubwa unaotegemewa na wananchi wengi ni wa boti?

Kutokana na uhalisia wa mazingira katika kisiwa cha Mafia, serikali kupitia TEMESA,  inapaswa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha usafiri wa uhakika unapatikana na kuwaondolewa adha wananyoipata kwa sasa. Majibu ya TEMESA ni mepesi kwa maswali magumu hasa kutokana na mazingira wanayokabiliwa nayo wananchi katika kisiwa cha Mafia.

Suala hili halipaswi kuchukuliwa kwa uzito mwepesi kama majibu yaliyotolewa bali kuchukua hatua stahiki kwa uzito mkubwa. Wananchi wa Mafia wanachohitaji si kuwataka wawe na uvumilivu bali majibu kwamba tatizo lao litashughulikiwa na kumalizika kwa namna gani.