Hongera CCM kuwabana wasiokubalika lakini...

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:22 AM Jul 17 2024
Wanachama wa CCM.
Picha: Mtandao
Wanachama wa CCM.

UCHAGUZI wa viongozi wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, ni wakati ambao Watanzania watachagua watakaowaongoza kwenye mitaa, vijiji na vitongoji kwa miaka mitano ijayo.

Wakati maandalizi ya uchaguzi yakiendelea, CCM inasema msimamo wake kuhusu uchaguzi huo, safari hii, haitaweka wagombea ambao si chaguo la wananchi.
 
 Sababu za kuja na msimamo huo, zinaelezwa na Katibu wa NEC, Siasa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla, kuwa ni kutokana na fundisho chama kilicholipata.
 
 Makalla anasema kimebaini kuwa mgombea anayekataliwa na kisha chama kikampitisha, anakuwa sio matakwa ya wapigakura na kwamba anaweza kusababisha chama kushindwa katika uchaguzi.
 
 Hatua hiyo ya CCM kuweka pembeni wagombea wasiokubalika inagusa kaulimbiu ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 iliyokuwa inasema; "viongozi bora wa serikali za mitaa ni chachu ya maendeleo."
 
 Makala anasema: "Tumeshaelezana Halmashauri Kuu za wilaya msibebe wagombea ambao siku mnamweka tu watu wanaanza kuguna. Tunaahidi kuweka wagombea bora, wanaokubalika na kuwatumikia wananchi.”
 
 Kwa kauli hiyo, ni wazi kwamba wagombea ambao hawana uwezo wa kuongoza au hawakuwa na nafasi tena ya kuwania uongozi ndani ya chama hicho katika uchaguzi ujao hawana nafasi.
 
 Lakini pamoja na hayo, ni vyema chama hicho pia kikajikita katika kudhibiti rushwa ambayo imekuwa ikidaiwa kuwapo wakati wa kampeni za kura za maoni na kusababisha wagombea wasio chaguo kushinda.
 
 Wakati huo ndio ambao  wanachama huwa wanalalamika kuwa baadhi ya wagombea hupenyeza rupia ili kukubalika kwa wajumbe na kwa wananchi na hatimaye kuibuka washindi.
 
 Hivyo, ili mkakati wa kuwaweka pembeni wagombea wasiokubalika na umma ufanikiwe, chama hakina budi kupenyeza watu wa kuwanasa wale watakaopenyeza rupia kwa lengo la kutaka wapitishwe kuwania uongozi.
 
 Miaka ya nyuma katika kura za maoni, baadhi ya wagombea ndani ya chama waliwahi kulalamikia uwapo wa kadi mpya zilizokuwa zinatolewa  kwa wasio wanachama ili wapige kura kumpa ushindi mgombea.
 
 Vilevile, kulikuwapo na mtindo wa kutotumia daftari lenye orodha halali ya wanachama, badala yake kila aliyekuwa anafika sehemu ya kupigia kura, aliruhusiwa ili mradi ana kadi ya chama.
 
 Baadhi ya viongozi wa chama wamekuwa wakituhumiwa kujihusisha na mchezo huo. Hivyo, wakati huu ambao CCM inakuja na mbinu mpya, ingeziba mianya hiyo ili lengo la kupata wagombea sahihi.
 
 Kwa mfano, mwaka 2022, CCM ilisimamisha uchaguzi katika mikoa mitatu kwa nafasi zilizoonyesha kuwa na changamoto na kufuta uchaguzi wa Umoja wa Vijana wa CCM kwa sababu ya rushwa.
 
 Hatua zilizochukuliwa na chama  wakati huo za kufuta uchaguzi, zinaonyesha kuwa wagombea wasio na sifa huwa wanatumia njia isiyo halali kupata nafasi, hivyo, CCM haina budi kujipanga zaidi.
 
 CCM ijipange kwa kuwafuatilia kwa karibu nyendo za watia nia, wajumbe na wanachama, ili kujiridhisha kama hakuna harufu ya rushwa ili hatimaye wapatikane wagombea ambao ni chaguo la wananchi.
 
 Njia hiyo ikitumika inaweza kuja na matokeo chanya, kwani baadhi ya wanachama wanaodai kwamba, wakati wa uchaguzi wapo wenzao ambao husema hawako tayari kumpa mtu kura akale bila kuwapa chochote.
 
 Wanaamini kwamba, wanapomchagua mtu katika nafasi ya uongozi, anakwenda kula, hivyo, wanaona ni bora nao wapate kitu kutoka kwa mgombea kuliko kumpa kura tu.
 
 Hongera CCM kuwabana wagombea wakubebwa  lakini ni vyema kama mtapenya kila kona kuwabaini wapigakura wa aina hiyo na wagombea wao, ili lengo la kupata viongozi wanaokubalika kwa wananchi litimie.