Dokta Omar shujaa wetu mpenda amani

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:35 AM Jul 10 2024
Hayati Dk. Omar Ali Juma.
Picha: Maktaba
Hayati Dk. Omar Ali Juma.

MAONESHO ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam, Sabasaba yanayofanyika Julai kila mwaka, hayawezi kumalizika bila kurejea kumbukizi za Makamu wa Rais wa awamu ya tatu, Dk. Omar Ali Juma.

Aliaga dunia Julai 4, 2001 wakati wa maonesho hayo yakiendelea, hadi leo anakumbukwa kwa kufanikisha uwepo wa uchaguzi wa vyama vingi ambao alikuwa mgombea mwenza wa Benjamin Mkapa mwaka 1995.

 Alifariki wakati serikali ya awamu ya pili ikiwa kwenye muhula wa pili baada ya kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi mkuu wa 2000.

 Miaka 23 iliyopita wakati wa maonesho ya Sabasaba kiongozi huyo alifariki dunia, saa chache baada ya kutoka kwenye viwanja vya maonesho Kilwa Road.

Julai 4 mwaka 2001 kabla ya kufariki dunia kiongozi huyo alitembelea mabanda mbalimbali katika maonyesho hayo, lakini muda mfupi baada ya kurejea nyumbani Oyster bay, habari za kifo chake zilisikika.
 
Tukio hilo liliwaacha Watanzania katika majonzi, huku wengine wakiwa hawaamini taarifa za kifo chake, hasa wale waliomshuhudia akitembelea mabanda mbalimbali kwenye viwanja vya Sabasaba.
 
Lakini, huo ndiyo ukawa mwisho wa miaka 60 ya safari ya Dk. Omar Ali Juma, hapa duniani, ambaye alizaliwa Juni 26 mwaka 1941 na kufariki dunia Julai 4 mwaka 2001.
 
Wakati huu wa kumbukumbu ya kifo chake, ni vyema pia kukumbusha na kuelezea machache kuhusu kiongozi huyo ambaye alidumu katika nafasi hiyo miaka sita.

Huyo ndiye alikuwa mgombea mwenza wa kwanza katika uchaguzi wa kwanza ndani ya mfumo wa vyama vingi uliofanyika 1995 na kuunda serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa.
 
Baada ya uchaguzi huo, Dk. Omar Ali Juma, akawa Makamu wa Rais wa kwanza ambaye marekebisho ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yalianzia kwake.
 
Marekebisho hayo yalikuja wakati nchi inajiandaa kufanya uchaguzi wa kwanza ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa ambapo mapendekezo ya marekebisho yalitokana na ushauri wa Tume ya Jaji Bomani.
 
Tume hiyo ilipendekeza kuwapo mgombea mwenza wa urais wa Jamhuri ya Muungano ambaye anakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuweka pembeni utaratibu kuwa Rais wa Zanzibar anakuwa Makamu wa Rais Jamhuri ya Muungano.
 
Kuanzia hapo hadi sasa, Rais wa Jamhuri ya Muungano na wa Zanzibar wanakuwa na mgombea mwenza ambaye ndiye Makamu wa Rais.

Unapozungumzia urejeshwaji wa mfumo wa vyama vingi, si rahisi kusahau jina la kiongozi shupavu Dk. Omar, kwa sababu unamgusa katika maeneo mbalimbali kuanzia marekebisho ya katiba.
 
Ni wa kwanza kuwa mgombea mwenza na hatimaye kushika nafasi ya Makamu wa Rais akianzia kwenye mfumo wa vyama vingi, ambavyo yeye na Mkapa walikuwa wahusika wakuu.

Wakati akiwatumikia Watanzania Dk. Omar Ali Juma, anayesifika kwa upole na unyenyekevu,  mambo mbalimbali yalijitokeza kwenye uwanja wa siasa za vyama vingi na kuibu mgogoro wa CCM na CUF kisiwani Pemba.

Akishirikiana na Mkapa hawakukaa kimya ili walisimamia na kukutana mezani ambako vyama CCM na CUF vilitiliana saini muafaka wa maridhiano  Juni 9, 1999 na kudhamiria kwa makusudi kutekeleza walichokubaliana na chini ya mpatanishi Jumuiya ya Madola.

Makamu wa Rais ofisi yake ilipewa jukumu rasmi la kutunza na kusimamia mazingira, akawa kiongozi anayeliongoza taifa kulinda mazingira kupambana na uharibifu na uchafuzi wa  kila aina.

Atakumbukwa kwa kuanzisha kampeni maalum ya kitaifa ya kupanda miti milioni kila mwaka, kampeni waliyoianza mwanzoni mwa  1999.
 
 Dk. Omar Ali Juma pia alipiga vita umaskini na uharibifu wa mazingira, hayo yalikuwa ni miongoni mwa mambo yaliyomkera huku akiamini kuwa umaskini una pacha ambaye ni uharibifu wa mazingira, na kwamba mama yao ni ujinga.
 
 Yapo mengi yanayomgusa kiongozi huyo, lakini kubwa zaidi likiwa ni la Makamu wa Rais wa kwanza kuhudumu katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, chini ya utaratibu wa kuwa na mgombea mwenza.