Mchengerwa: Uandikishaji Uchaguzi Serikali za Mitaa umefanyika vizuri

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:14 PM Oct 21 2024
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa.
Picha: Mtandao
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa.

WAPIGAKURA 26,769,995 sawa na asilimia 81 ya lengo la kuandikisha wapigakura 32,987,579, wameandikishwa kwenye daftari la wapigakura wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hadi kufikia juzi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, aliyasema hayo jana alipokuwa anatoa taarifa ya mwenendo wa uandikishaji wapigakura, kwa ajili ya uchaguzi huo kwenye Halmashauri ya Rufiji, mkoani Pwani. 

Alisema hali ya uandikishaji wapigakuwa kwa siku tisa ni nzuri na jumla ya wapigakura 26,769,995 walikuwa wamejiandikisha kupiga kura sawa na asilimia 81.15 ya lengo la kuandikisha watu 32,987,579 kwa siku zote 10.

 "Jumla ya uandikishaji kwa wanaume ni 13,033,988 sawa na asilimia 48.69 ya watu wote waliojiandikisha kwa tarehe 11-19 Oktoba, 2024 na wanawake ni 13,736,007 sawa na asilimia 51.31 ya watu wote waliojiandikisha," alisema. 

Waziri huyo alisema kuwa kwa ujumla, mwenendo huu ni mzuri na unaridhisha na kwamba kuanzia siku ya tano hadi ya tisa kulikuwa na ongezeko la idadi ya Watanzania waliojitokeza kujiandikisha.

 Mchengerwa alitaja mikoa mitano yenye asilimia kubwa ya uandikishaji hadi kufikia tarehe 18 Oktoba, 2024 kuwa ni Tanga asilimia 101.13, ulifuatiwa na Pwani asilimia 98.74 kisha Mwanza asilimia 94.09, Dar es Salaama asilimia 86.66 na Dodoma asilimia 80.63 ya malengo. 

Mchengerwa alisisitiza kuwa hakuna siku zitakazoongezwa kwa ajili ya uandikishaji wapigakura. Tarehe 20.10.2024, yaani jana saa 12:00 jioni ndiyo mwisho wa uandikishaji.