Pombe kali zaongeza wagonjwa moyo mikoa Kanda ya Kaskazini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:25 PM Oct 21 2024
Pombe kali.
Picha:Mtandao
Pombe kali.

IDADI kubwa ya wagonjwa wa moyo wanaotoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga, wanapata maradhi hayo kutokana na unywaji wa pombe kali uliopitiliza, wataalamu wamebaini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Peter Kisenge alisema mwishoni mwa wiki kuwa Kanda ya Kaskazini inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa moyo nchini, akikitaja chanzo hicho kinachoongezwa msukumo na watu kutofanya mazoezi.

Dk. Kisenge alikuwa akitoa mrejesho kuhusu huduma za kibingwa zilizotolewa na serikali katika kambi ya siku tano ya matibabu jijini Arusha.

"Ndugu zangu, ugonjwa wa moyo husababishwa na unywaji wa pombe kali, lakini pia kutokufanya mazoezi, nayo ni sababu nyingine.

"Niwaombe wananchi hususani kanda hii ya kaskazini, mfanye mazoezi walau muwe na muda wa kutembea kama hakuna umbali wa kupanda gari au pikipiki. Ni vyema ukatembea, inapunguza kwa kiasi kikubwa moyo kutanuka," alisema Dk. Kisenge.

Alieleza sababu ya kurudi Arusha kuweka kambi ya matibabu, ni kuendelea kuimarisha utalii, lakini pia kuvutia kufanya maandalizi ya kufungua Kituo cha JKCI Arusha, ili kujiandaa kwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.

Aliwataka wananchi kuwa na kawaida ya kupima afya zao, ili kubaini tatizo mapema na kulishughulikia, huku akieleza kuwa matibabu ya magonjwa ya moyo kwa hatua ya juu, hutumia gharama kubwa kuanzia Sh. milioni sita hadi 10.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC), Dk. Godwin Kivuyo, alishukuru serikali kwa kuweka miongozo na sera za ubia kati ya taasisi za kidini na binafsi kuhakikisha suala la afya linakuwa na ahueni kwa wananchi kwa kupunguza gharama za matibabu.

"Ninashukuru serikali kwa kuweka miongozo na sera nzuri za ubia. Hili limetuwezesha kuingia makubaliano na JKCI kufanya kambi ya matibabu mwaka 2022 na mwaka huu, kwetu ni jambo la kushukuru," alisema.

Wakizungumzia kambi hiyo wagonjwa wanaoendelea kupatiwa huduma, wameeleza unafuu wanaopata katika huduma hiyo, huku wakisisitiza kuwa kufuata huduma hiyo jijini Dar es Salaam, uliwafanya wengi kushindwa kumudu gharama za usafiri na malazi.

Theresia Joel, mkazi wa Arusha, alisema kwao ni nafuu kusogezewa huduma hiyo karibu, akieleza kuwa kuifuata Dar es Salaam ni gharama mara mbili  kutokana na gharama za nauli, malazi na chakula.

Akundaeli Kweka, mkazi wa Siha, mkoani Kilimanjaro, alisema kutokana na wagonjwa wengi kuwa na hali duni ya maisha, hulazimika kusalia nyumbani na kujitibu kwa kutumia dawa za kutuliza maumivu, huku wakishindwa kuhudhuria kliniki ya moyo.