WAKOPESHAJI MTANDAONI; Hawatambuliki BoT wala BRELA, uendeshaji umejaa udhalilishaji-1

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:56 PM Oct 21 2024
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel  Tutuba.
Picha:Mtandao
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba.

SIKU 36 baada ya mwandishi wa gazeti hili kuwasilisha maswali Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kutaka kujua kwanini wakopeshaji mitandaoni wanadhalilisha wakopaji, taasisi hiyo imetengeneza mwongozo kwa watoa huduma ndogo za fedha wa daraja la pili, wanaotoa huduma za mikopo kidijitali.

Agosti 19 mwaka huu, mwandishi wa habari hii aliwasilisha maswali BoT akitaka kujua, pamoja na mambo mengine, kama taasisi/kampuni zinazotoa mikopo mtandaoni zinatambuliwa na BoT na hatua inazochukua dhidi ya wakopeshaji wanaodhalilisha wakopaji.

Septemba 2, mwaka huu, BoT ilijibu maswali hayo, ikieleza kuwa haitambui taasisi hizo na kwamba imeshatoa tangazo kwa umma la katazo la kuendesha mikopo hiyo, mpaka watakapopata kibali cha BoT.

Katika majibu yake kwa mwandishi, BoT ilieleza kuwa Sheria ya Watoa Huduma Ndogo za Fedha, inaruhusu kutoa mikopo kwa njia ya mtandao, lakini mpaka wapewe kibali cha taasisi hiyo, ingawa hadi wakati huo hakuna hata mkopeshaji mmoja wa mtandaoni aliyekuwa amesajiliwa.

 BoT pia ilithibitisha kumekuwa na malalamiko ya matumizi mabaya ya taarifa za waombaji mikopo ya mtandaoni.

Septemba 24, mwaka huu, ikiwa ni siku 36 tangu mwandishi wa Nipashe awasilishe maswali BoT, Naibu Gavana Dk. Yamungu Kayandabila, alitoa taarifa kwa umma kuwa wamechapisha Mwongozo wa Watoa Huduma za Fedha wa Daraja la Pili, wanaotoa huduma za mikopo kwa njia ya kidijitali.

Alisema kuwa mwongozo huo wa mwaka 2024 una lengo la kuimarisha usimamizi wa uendeshaji huduma za mikopo kidijitali.

 "Mwongozo huu unalenga kuhakikisha uzingatiwaji kanuni za kumlinda mlaji wa huduma za kifedha, ikijumuisha uwazi, uwekaji bei, njia za ukusanyaji madeni, utunzaji taarifa za wateja na faragha.

 "Kufuatia mwongozo huu, BoT inawaelekeza watoa huduma ndogo za fedha wa daraja la pili wanaotoa au wanaokusudia kutoa mikopo ya kidijitali, kutii matakwa ya mwongozo huu.

"Endapo mtoa huduma atakiuka agizo hili, BoT itachukua hatua za kiutawala, ikiwamo faini, kusitisha shughuli za utoaji mikopo ya kidijitali na kufutiwa leseni ya kuendelea na biashara ya huduma ndogo za fedha. BoT itachapisha orodha ya watoa huduma walioidhinishwa kutoa huduma kidijitali," alisema.
 
 UCHUNGUZI WA NIPASHE

 Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa Nipashe kwa miezi minne, umebaini utoaji mikopo mtandaoni kiholela. Ni mikopo yenye riba kubwa inayofika hadi asilimia 80, masharti ya mikopo yanafichwa, udhalilishaji wakopaji kwa kuundiwa makundi katika mitandao ya kijamii kisha picha zao kusambazwa, matumizi ya namba za simu zenye utambulisho (code) usiotambulika.

Fedha ya Tanzania.

Mwandishi pia amebaini vijana wenye umri mdogo wamekuwa wanatumika kutukana na kudhalilisha wakopaji kwa njia ya simu, kutuma na kusambaza picha chafu zilizotengenezwa kwa lengo la kushinikiza mkopaji kulipa kiasi kisichostahili, wakopaji kupewa mkopo pungufu kinyume cha makubaliano ya awali na kuwapo raia wa kigeni wanaotumia teknolojia kutoa mikopo.

Katika uchunguzi wake, mwandishi pia amebaini wakopeshaji wana watumishi wanaodai kulipwa ujira kwa kadri wanavyokusanya, ofisi feki za wanaotoa mikopo na matangazo yenye udhamini katika mitandao ya kijamii ya Facebook na Instagram.

 Vilevile, mwandishi amebaini kuwa mara baada ya mkopaji kutoa rukhsa ya taarifa zake binafsi kujulikana, wakopeshaji wanakuwa na uwezo wa kuingia katika akaunti yake ya Google na kuona mawasiliano yote kisha hutuma ujumbe ndani ya dakika moja, kwa watu wote walio katika orodha ya simu ya mkopaji kuwaarifa kuwa "huyu anadaiwa".

Uchunguzi pia umebaini wakopeshaji wanaingilia na kuendesha mawasiliano ya mtu, jambo ambalo limekuwa chanzo cha utapeli ukiwamo wa "zile fedha tuma katika namba hii".

Wakopeshaji hao wanakwenda mbali zaidi, kuna wakati wanavunja ndoa na baadhi ya watu kuripotiwa kujiua kutokana na madeni yasiyolipika; yanakuwa na riba inayoongezeka bila ufafanuzi rasmi.


 Mwandishi alibaini hakuna mwongozo wala sheria ya kuwadhibiti hadi BoT ilivyotangaza mwongozo huo Septemba, mwaka huu. Ni hatua iliyopunguza kasi ya matangazo ya wakopeshaji hao katika mitandao ya kijamii, lakini baada ya wiki moja, matangazo hayo yalirejea kwa kasi. 

Katika uchunguzi huo, ilibainika kuwa wakati wa kurejesha mkopo, namba inayopokea fedha imesajiliwa kama taasisi ndogo ya fedha. Mathalani, mkopaji aliyekopa kwenye App ya Bahari, aliporejesha, namba ilisoma ametuma kwa Stormtime Microfinace Company Limited.
 
 BRELA: HATUWATAMBUI 


 Katika orodha ya 'applications' 21 za wakopeshaji ambazo mwandishi alifuatilia, hakuna iliyosajiliwa kwa jina tajwa (Stormtime Microfinace Company Limited) wala kutambuliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
 

Godfrey Nyaisa, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA
Mwandishi aliingia katika mfumo rasmi wa BRELA wa kuangalia usajili wa kampuni na hakufanikiwa kupata kampuni yoyote yenye jina linalotumika mtandaoni kutoa mikopo.

Septemba 23, mwaka huu, Msajili wa Kampuni wa BRELA, Leticia Zavu, alisema walifanya mapatio katika Daftari la Msajili wa Kampuni na Daftari la Usajili wa Majina ya Biashara, lakini hawakuona majina yaliyoorodheshwa kwenye barua ya mwandishi wa gazeti hili aliyetaka kujua usajili wa Stormtime Microfinace Company Limited, App ya Bahari na nyinginezo ambazo mwandishi alikuwa anataka taarifa za usajili wake.

Katika barua yake kwa BRELA, mwandishi alikuwa na orodha ya majina ya wakopeshaji wafuatao wa mtandaoni: Mkopo wako; PesaX Tanzania; PataPesa-Instant Loans; OKOA MAISHA Finance, HiPesa-Mkopo Haraka Fast Loan; Fundflex; SwiftFunds; CashX: Online; BobaCash-Pesa&Usalama; GetLoan-Finance; Matupesa-Haraka Cash LoanFinance.

Wengine ni: Mkopo Huru; Branch: Quick Online Loan App; Flexi Cash-mkopo wa fedha; FinLoanOSafety, NoHiddenFees; TikCash, OnePesa; BahariPesa-Mikopo ya Mikopo Finance, Furaha Loan; na Zima Cash-instant Cash Loan.

Msajili Leticia alisema kuwa katika orodha hiyo iliyowasilishwa na mwandishi, walipata alama mbili za biashara ambazo ni Branch na Onepesa, na kwamba Branch inamilikiwa na Branch International Limited na imesajiliwa kwa kutoa huduma za fedha, bima na mali zisizohamishika (Real Estate), huku Bahari ikiwa na viashiria vya kuwa na uhusiano kibiashara na Stormtime Microfinance Company Limited.


 Kwa mujibu wa msajili huyo, ufuatiliaji wao ulibaini Onepesa inamilikiwa na Mrisho Omari Sultani Trading as Baromo Micro-Credit na inatoa huduma za mikopo. Maombi ya usajili yameshapokewa na ilitangazwa siku 60 za mchakato wa usajili.


 "Upekuzi umeonesha baadhi ya majina yanakaribiana na majina yaliyosajiliwa BRELA. Hivyo inawezekana wahusika wanajitambulisha kwa majina ambayo ni tofauti na yale ambayo yamesajiliwa na wanatumia majina kwa kufupisha. 

"Kutokana na hali hii, tunashauri wateja kuhakikisha wanajiridhisha na uhalali wa usajili wa kampuni na majina ya biashara, kabla ya kuingia makubaliano yoyote ya kibiashara.
 "Kutokana na watu wengi kujitambulisha kama kampuni zilizosajiliwa kutoa huduma za mikopo mitandaoni, tunapenda kuwakumbusha Watanzania kuwa huduma ya kupata uthibitisho wa usajili wa kampuni au jina la biashara, inapatikana kwa njia ya mtandao, yaani Online Registration System (ORS).

"Hivyo, wanatakiwa kutumia mfumo huo, ili kuzitambua kampuni halali zilizosajiliwa kutoa huduma kabla ya kufanya makubaliano yoyote," Msajili Leticia alisema.

Msajili Msaidizi wa BRELA, Seka Kasera, alisema ni lazima kuwe na msimamizi wa huduma ya mikopo inayotolewa, ili kuwa na usalama kwa wanaochukua na kutoa mikopo, baadhi ikiambatana na matangazo kwamba ndani ya dakika 15 mtu anapewa mkopo.

*ITAENDELEA KESHO