Kunenge ataka mashirika ya umma kufuata vipaumbele vya Rais

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 07:44 PM Oct 21 2024
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.
Picha: Mpigapicha Wetu
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema mashirika ya umma yanatakiwa kufanya kazi kwa kufuata vipaumbele vya Rais kwani wao ndio watekelezaji wa mambo ambayo yanatakiwa kuleta matokeo chanya.Kunenge ameyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya Uongozi na Menejimenti kwa viongozi wa wa Mashirika ya Umma yanayofanyika katika shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Kwamfipa Kibaha.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema Rais Samia Suluhu Hassan kuna mambo ambayo anatarajia yatokee kulingana na vipaumbele vyake na mashirika ya umma ndio yanatakiwa kufanya hivyo kwa kujipanga katika utendaji wao.

"Lazima ujue vitu gani utafanya vilete tija, lazima uweke malengo  na kufanya tathmini kutokana na wateja unaowahudumia na hii sio kwa mashirika ya umma pekee hata kwa watumishi wa Serikali Kuu lazima ujue unachofanya kinaendana na vipaumbele vya Rais (Samia)," amesema.

Amezikumbusha taasisi hizo pia kujua wateja wao ni akina nani na kuachana na tabia ya kujifungia ndani na kujiaminisha kwamba wanafanya kazi nyingi na badala yake wawe na mabadiliko katika utendaji wao kwa kufanya kazi kuendana mazingira ya kimataifa.

Kunenge pia amesema mashirika hayo yanatakiwa kufanya kazi zao kwa ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi sambamba na kuwezesha kujiendesha yenyewe  bila kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu.

Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Profesa Marcellina Chijoriga amesema ni wakati sasa wa viongozi wa Mashirika ya Umma kuwa na mabadiliko katika utendaji wao sambamba na kuwa wazalendo.

"Tunategemea katika shule yetu kutoa mafunzo kwa viongozi mbalimbali na kwa upande wa Taasisi za Umma tunalenga kuwabadilisha viongozi wake kutokana na umuhimu wake wengi mmeona baadhi ya mashirika yamekufa na mengine hayafanyi vizuri," amesema.

Profesa Chijoriga amesema sasa ni wakati wa kujidhatiti mashirika ya Umma yaweze kufanya kazi kwa uzalendo na ufanisi kukidhi malengo kwa kutoa huduma zinatolewa kwa ufanisi.