Waziri Lukuvi- Rais Samia ametutendea wema wananchi wa Isimani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:35 PM Oct 21 2024
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) William Lukuvi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) William Lukuvi, Mbunge wa Isimani amemushukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kijiji cha Msembe lango la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha mpaka Iringa Mjini.

Waziri ametoa shukrani hizo wakati wa ziara yake katika kata ya Idodi ya kutembelea miradi ya maendeleo ambapo pia amepata fursa ya kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika kitongoji cha Msimbi kilichopo katika kijiji cha Idodi jana Agosti 20,2024.

Alifafanua kwamba Ujenzi wa barabara hiyo ni shauku ya watu wa Jimbo la Isimani waliyokuwa nayo kwa muda mrefu na kampuni ya Chicco ndio imeshinda tenda ya ujenzi wa kipande hicho cha barabara.
Waziri Lukuvi amesema, “barabara hiyo itaajiri Watanzania kwa shughuli watakazoweza kufanya na Miji yetu Mikubwa ya Tungamalenga, Idodi, na Mapogoro itawekwa taa za barabarani.”

Aidha kwa upande wa Isimani Serikali imejenga miuundo Mbinu ya maji na kusaidia wananchi wa Tarafa ya Isimani kupata maji safi, kwa kutoa Maji kutoka Kilolo na Kuleta Isimani na kuchukua Maji kutoa Iringa Mjini na Kuleta Isimani hivyo kila kijiji kinapata huduma ya maji safi na salama.

Waziri Lukuvi alisema katika eneo la Pawaga Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mfereji mkubwa wa umwagiliaji na hivyo kusaidia mashamba makubwa ya umwagiliaji katika eneo hilo kwa kusaidia shughuli za kilimo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.

“Mhe. Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan ametufanyia wema mkubwa watu wa Isimani kwa kutimiza shauku ya kupata mambo tuliyokuwa tunahitaji katika kipindi chake kifupi cha miaka mitatu, alisema.

Kwa upande wake Diwani wa Idodi, Julius Mbuta alisema anaishukuru serikali kwa kuleta fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika kata ya Idodi, na kuondoa changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama.
“Ukarabati wa miundo mbinu ya barabara umesaidia maeneo mengi katika kata ya Idodi kufikika kirahisi hivyo kusaidia wananchi kurahisisha mawasiliano kutoka eneo moja kwenda eneo jingine” alisema Mbuta.