LHRC yalaani utekaji, udhalilishaji wa Aisha Machano

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 08:51 PM Oct 21 2024
LHRC yalaani utekaji, udhalilishaji wa Aisha Machano.
Picha:Mpigapicha Wetu
LHRC yalaani utekaji, udhalilishaji wa Aisha Machano.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani vikali kitendo cha utekaji, udhalilishaji, na kupigwa kwa Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) Taifa, Aisha Machano. Kituo hicho kimesema kuwa kitendo hicho kinakiuka mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania ni mwanachama.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 21, 2024, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga, alisema kuwa kituo hicho kinashutumu vikali vitendo hivyo vya utekaji na ukatili ambavyo vimekuwa vikishamiri nchini wakati huu wa kuelekea uchaguzi.

Dk. Henga ametoa wito kwa vyombo vya dola kuhakikisha wanawasaka na kuwakamata wahusika wa vitendo hivyo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ili hatua stahiki zichukuliwe. Alisema, “Tunataka vyombo husika kufuata sheria pindi vinapowakamata wahusika wa uhalifu, na wahakikishe wanawafikisha mahakamani ndani ya muda uliowekwa kisheria.”

Amebainisha kuwa katika kipindi cha karibuni, kumekuwepo na matukio mengi yanayokiuka haki za binadamu katika maeneo mbalimbali nchini, jambo ambalo LHRC haiwezi kulifumbia macho.

Dk. Henga ameeleza kuwa leo, Oktoba 21, ni Siku ya Haki za Binadamu Afrika, na ni jambo la kusikitisha kuona Tanzania ikiadhimisha siku hiyo huku kukiwa na matukio mengi yanayovunja haki za binadamu.

Ameongeza kuwa, kupitia taarifa mbalimbali kutoka kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kumekuwa na ongezeko la matukio ya uvunjaji wa haki za binadamu na utawala bora, hususan kukamatwa kwa viongozi wa vyama vya siasa bila kufuata utaratibu wa kisheria.

Ameongeza, “Vitendo vya kunyanyasa na kuumiza wanawake, hasa wale wanaojihusisha na siasa katika kipindi hiki cha uchaguzi, ni kinyume na sheria na haki za binadamu.”

Akitolea mfano, Dk. Henga amerejelea tukio la Oktoba 18, 2024, ambapo Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Katavi, Rhoda Kunchele, alikamatwa pamoja na Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Iringa Mjini, Frank Nyalusi, ambao baadaye walitolewa kwa dhamana na Jeshi la Polisi.

Kuhusu Aisha Machano, inadaiwa kuwa alitekwa na watu sita huko Rufiji, mkoani Pwani, akapigwa, kuteswa, na baadaye kutupwa porini. Alijikuta akiwa hospitali ya Rufani ya Mwananyamala, Dar es Salaam, baada ya kuokolewa.