Hifadhi ya Ruaha yaonya wafugaji kuingiza mifugo Bonde la Ihefu

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 06:14 PM Oct 21 2024
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Godwell Ole Ming’ataki.

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA), limeonya baadhi ya watu wanaowapotosha wafugaji wilayani Mbarali katika Mkoa wa Mbeya kwamba Serikali imeruhusu kuingiza mifugo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha likidai kuwa taarifa hizo sio za kweli na litachukua hatua.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Godwell Ole Ming’ataki ameyasema hayo alipozungumza na wandishi wa habari kuhusu tatizo la makundi ya mifugo kuingizwa ndani ya hifadhi hiyo katika kipindi hiki cha ukame.

Amewataka wafugaji kutokubali kurubuniwa na watu hao wasiokuwa na nia njema akidai kuwa wanaendelea na doria mbalimbali za angani na za kutembea kwa miguu ndani ya hifadhi hiyo kusaka mifugo hiyo.

Amesema wakiikamata mifugo hiyo wataendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kuwapeleka mahakamani na kuitaifisha hali ambayo itawasababishia hasara wafugaji hao.

Amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wafugaji katika maeneo mbalimbali wilayani humo ili waelewe umuhimu wa hifadhi hiyo na kuacha kuingiza mifugo.