Mchechu aongoza waumini kuchangia ujenzi wa kanisa

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 05:45 PM Oct 21 2024
MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu.
Picha:Mpigapicha Wetu
MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu.

MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu, ameendesha harambee kuchangisha Sh. milioni 117.8, ili kuendeleza ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Naibili, Siha, Kilimanjaro.

Katika harambee hiyo ya jengo la ibada, ujenzi wake ambao ulianza miaka sita iliyopita, zimchangwa Sh. milioni 50.2 taslimu; Sh. milioni 66.5 ahadi na Sh. milioni 1.1 zikipatikana kwa njia ya mnada.

Katika harambee hiyo iliyofanyika Jumapili, Oktoba 20, 2024, pia ilipatikana mifuko 118 ya saruji.

Pesa hizo na saruji ni kwa ajili ya upanuzi wa jengo hilo la ibada na kazi ya plasta, kwa mujibu wa Askofu Dk. Fredrick Shoo, Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT.

Akizungumza na viongozi wa dini, serikali na jamii, pamoja na waumini wa Naibili, Mchechu alieleza haja ya kuendelea kuwa na moyo wa kutoa na kushirikiana mpaka ujenzi utakapokamilika.

 â€śTunapoendelea na ujenzi huu, nataka niwaombe ninyi wapendwa msiishie hapa. Tuendelee kufanya kazi kwa pamoja mpaka ujenzi utakapokamilika,” alisema.

“Kanisa bado linahitaji michango yenu, maombi yenu, na utayari wenu wa kujitoa. Kila mmoja wetu anaweza kutoa kitu, iwe ni fedha, muda, au huduma kwa namna yoyote ile.”

Alisema ikiwa watatoa kwa moyo wa upendo, Mungu atarudisha zaidi na zaidi na vikombe vyao vitafurika, huku akinukuu kitabu kwenye Biblia: Luka 6:38: Wapeni watu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa, cha kusukwasukwa, na kushindiliwa, na kufurika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu.

1

“Kama vile Nehemia alivyowaongoza watu wa Yerusalemu kujenga tena ukuta wa mji baada ya kuharibiwa, ninyi pia muendelee kujitoa kwa uaminifu na bidii katika ujenzi wa nyumba ya Mungu.”

Kwa upande wa Dk. Shoo, alisema matamanio yao ni kuona wanakamilisha plasta, kuweka madirisha, milango na madhabahu, kupaka rangi na kuanza maandalizi ya kutengeneza samani, ifikapo mwaka 2026.

Mpaka kufikia hatua ya ujenzi huo, Sh. milioni 229.8 zimetumika.

Askofu Dk. Shoo alisema baada ya upanuzi na plasta, awamu ya pili ni kujenga madhabahu na madirisha na milango ya mbao.

“Baada ya hapo awamu inayofuata itakuwa kuweka tarazo, bodi ya dari, kusuka umeme na rangi, huku awamu ya nne, ikiwa ni kuweka viti na kumalizia madhabahu kwa kutumia mbao.

“Ni wakati mwafaka wa kushirikiana kufanya kazi hii ya baraka iliyopo mbele yetu. Mungu atutie nguvu.”