Kigogo CHADEMA: Nilitekwa, nikateswa

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 01:01 PM Oct 21 2024
KATIBU Mwenezi wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) Taifa, Aisha Machano.

KATIBU Mwenezi wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) Taifa, Aisha Machano anayedaiwa kutekwa, kupigwa kisha kutupwa katika pori ameeleza namna tukio hilo lilivyofanyika hadi kujikuta akiwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa Mwanayamala, Dar es Salaam.

Taarifa ya tukio hilo ilitolewa jana asubuhi na CHADEMA kupitia mitandao ya kijamii, chama hicho kikilihusisha na kitendo cha BAWACHA kuchoma vitenge vyenye picha ya Rais Samia Suluhu Hassan, wiki mbili zilizopita.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Aisha alisema kuwa juzi saa saba mchana, alipatwa na baa hilo akiwa wilayani Kibiti, mkoani Pwani, akitekeleza majukumu ya kichama ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kugombea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Aisha alisema kuwa akiwa katika kituo cha daladala cha Bungu, alikutana na mwanamke ambaye alimchukulia kama abiria wa kawaida. Alipopanda katika basi na kukaa kiti cha mwisho, mwanamke huyo naye alipanda na kwenda kukaa karibu yake.

Wakiwa wanaendelea na safari, alilipa nauli na kumwelekeza utingo kuwa anashuka kituo kinachoitwa Jaribu na mwanamke huyo naye alilipa nauli na kuelekeza kuwa anashuka kituo hichohicho. Walipofika kituoni, mwanamke huyo alitangulia kushuka kisha naye akafuata nyuma yake.

Alidai kuwa wakati anavuka barabara kuelekea upande wa pili, kwa ajili ya kupanda bodaboda, lilikuja gari aina ya Landcruiser ambalo namba zake zinaanza na PT kisha wakashuka wanaume sita.

"Mmoja wao akaja akanigusa bega, akaniambia 'upo chini ya ulinzi, sisi ni polisi'. Nikamwambia 'ninaomba kitambulisho', akawa mkali. Wenzake wakaniambia 'ingia kwenye gari haraka, tunataka tuondoke, kuna mwanamke huyu hapa'. 

"Wakati ninamwangalia yule mwanamke, nikagundua kuwa ni yule niliyepanda naye gari na kushuka naye," Aisha alisimulia.

Alidai kuwa alipoingia kwenye gari, yule mwanamke alimfunga pingu na mwingine (mwanamume) akimfunga kitambaa cheusi usoni kisha wakaanza safari ndefu saa 7:30 mchana na walifikia katika msitu ambao hakuutambua majira ya jioni.

Kwa mujibu wa Aisha, walipofika msituni, walimshusha na kumweka katika mti kisha wakaanza kumpiga kwa magongo sehemu mbalimbali za mwili, huku wakimwuliza ni nani aliyemtuma achome vitenge.

"Mimi nikawaambia kuwa sikutumwa, mimi ni kiongozi wa BAWACHA taifa, hivyo tuliandaa sisi viongozi na viongozi wetu wa mikoa tukafanya hilo tukio la kuchoma vitenge, na tulichoma kwa sababu kuna mambo yetu tulimwomba Rais Samia ayafanyie kazi, lakini hakuyafanyia kazi, ikiwamo vijana wetu watano waliopotea," alidai.

Alisema majibu hayo hayakuwaridhisha watu hao kwa kuwa waliendelea kumpiga na kumwambia kuwa kama asipowaeleza ukweli, wangemmaliza siku hiyo na kumlazimisha akiri kuwa walitumwa na viongozi wao wa chama.

Alitaja maelekezo mengine aliyodai walimpa ni kuwataja viongozi wa CHADEMA waliohudhuria mkutano na waandishi wa habari aliofanya hivi karibuni, Dar es Salaam na pia walimwuliza sababu za Katibu wa chama Mkoa wa Dodoma, kushiriki mkutano huo.

Baada ya kipigo cha muda mrefu, Aisha alidai walimfungua pingu na kitambaa kisha wakamvua nguo zote na kumpiga picha, wakamtishia kuwa akiitisha kikao na waandishi wa habari na kueleza yaliyotokea, watammaliza kabisa na kusambaza picha zake za utupu.

Alidai kuwa baadaye walimpandisha kwenye gari na kwenda kumshusha eneo lingine ambalo pia halifahamu kisha wakampa vitu vyake. Baada ya gari kuondoka, alinyanyuka na kufuata njia lilimopita gari hilo, huku akiwa anahisi maumivu makali na njaa.

Aisha alidai kuwa alitembea kwa muda mpaka akatokea eneo lenye kibanda cha kuuza chipsi na madereva wa bodaboda kisha akapoteza fahamu na alipozinduka, alijikuta yuko katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa Mwanyamala, Dar es Salaam na madaktari wakamweleza kuwa alipelekwa huko na bodaboda waliomwokota wilayani Kisarawe.

Alisema kuwa baada ya kuwaeleza madaktari, mkasa uliomkuta na kuwaonesha majeraha aliyonayo, aliandikiwa kuchukua vipimo vya X-ray ambavyo vilionesha kuwa hana majeraha yoyote makubwa ya ndani kama vile mfupa kuvunjika.

Aisha aliwaeleza BAWACHA kuwa wasikatishwe tamaa na tukio liliompata, bali waendelee kuhamasisha wanawake kujitokeza kugombea nafasi na kupigakura katika uchaguzi ujao.

KAULI YA POLISI

Jeshi la Polisi lilithibitisha kupokea taarifa ya kuokotwa kwa kiongozi huyo wa CHADEMA na limeanza uchunguzi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

"Tunatoa wito kwa wananchi watulie, uchunguzi utatoa majibu sahihi ya nini kilichotokea dhidi yake, sababu zake ni zipi, wahusika ni nani na hatua zitachukuliwa kulingana na ushahidi utakaopatikana, kwa mujibu wa sheria," inasomeka sehemu ya taarifa ya Msemaji wa Jeshi Polisi nchini, DCP David Misime.