Utafiti wabaini ongezeko vijana wa kiume kulawitiwa

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 09:40 AM Oct 21 2024
Utafiti wabaini ongezeko vijana wa kiume kulawitiwa
Picha: Mtandao
Utafiti wabaini ongezeko vijana wa kiume kulawitiwa

UTAFITI uliofanywa kwa siku tisa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na wanajamii wanaotoka vijiji vinane vya kata ya Mabogini, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, umebaini ongezeko la ukatili wa kingono, hasa ulawiti kwa vijana wa kiume katika eneo hilo.

Maeneo ya Kwa Manosa na Bogini Juu yametajwa ndiko ukatili huo unaendelea, vijana wa kiume wakilawiti kwa kundi, ambapo ndani ya wiki moja mwezi uliopita, matukio hayo yalijitokeza mara mbili.

Matokeo ya utafiti huo wa TGNP na Kituo cha Taarifa na Maarifa-Kata ya Mabogini, yaliwasilishwa mwishoni mwa wiki na Benard Massawe kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Lukas Mselle.

Mselle na timu yake ya baadhi ya wakuu wa idara za halmashauri hiyo, walipokea utafiti huo na kushauri baadhi ya mambo ambayo Kituo cha Taarifa na Maarifa kinapaswa kuongeza katika ripoti yao, ili kusaidia serikali kuchukua hatua.

Maeneo tishio kwa ukatili wa kingono, hasa ulawiti na ubakaji yametajwa ni vijiji vya Mserekia, Mabogini, Chekereni, Muungano na Maendeleo, huku ndoa za utotoni zikionekana kuwa mwiba zaidi eneo la Remiti, kijiji cha Mserekia.

Pamoja na mambo mengine, utafiti huo umebaini vijana hao huungana na kusubiri watu walewe pombe na baada ya hapo humchukua mtu huyo, ambaye wamepanga kwamba ni siku yake kulawitiwa na hufanya hivyo huku wakimrekodi kwa kumpiga picha jongefu (video).

"Kuna vijana wengi wanalawitiwa na wa kike wamekuwa wakibakwa katika maeneo hayo. Wako wanafunzi wanaachishwa shule na kuozwa katika umri mdogo; umri ambao si sahihi kuolewa. Maeneo watoto wanaolewa ni Remiti, kijiji cha Mserekia. Maeneo hayo yamekuwa yanaathiriwa zaidi na ukatili huu.

"Wanafunzi wengi wamekuwa wakitoka majumbani kufuata elimu maeneo ya kijiji cha Chekereni, mahali penye umbali mrefu; ukizingatia watoto wanakutana na changamoto mbalimbali na huko kuna mapori katikati.

"Pia katika vijiji vyetu kumekuwa na ukatili unaotokana na matumizi makubwa ya dawa za kulevya, ikiwamo bangi na mirungi. Kijiji cha Mabogini kimeathiriwa na dawa hizi hasa kituo kidogo cha mabasi ya abiria cha Chekereni.

"Wakishatumia dawa za kulevya, wanakwenda kufanya ukatili wa kijinsia katika jamii zetu. Vijana wengi wamekuwa wakikutana maeneo hayo na biashara hizo zimekuwa zikiendelea na watumiaji wamekuwa wakipatikana maeneo hayo," alisema.

Kata ya Mabogini inaundwa na vijiji vya Mvuleni, Mji Mpya, Maendeleo, Chekereni, Muungano, Mabogini, Mtakuja na Mserekia.

Ofisa na Mwezeshaji wa TGNP, Agness Rukanga, alisema Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ni kati ya halmashauri ambazo zina ukatili mkubwa, hasa  kata  ya Mabogini kutokana na kutajwa katika utafiti wa  Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF). 

"Katika ngazi ya kata, tumepata mapokeo mazuri na ushirikiano mzuri sana na uongozi wa kata umeahidi baada ya kumalizika shughuli za uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, wanatamani kukaa na kundi zima, ili kutafuta njia ya kutatua zile changamoto ambazo zimeibuliwa.

"Tupo hapa kujitambulisha kwamba TGNP tupo. Mjue tuna hiki kituo na mtashirikiana nao katika utendaji, hasa suala zima la bajeti katika mrengo wa kijinsia au katika uchambuzi wa miongozo, kanuni mbalimbali na jicho la kijinsia. Ninaamini watakuwa ni washiriki wazuri na kwa njia moja au nyingine wanaweza kuishauri halmashauri," alisema.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Moshi, Mselle, akijibu hoja kuhusu utafiti huo, alisema yote yaliyoibuliwa atayafikisha kwa Mkurugenzi wake, Shadrack Mhagama, kwa kuwa serikali inaamini TGNP ni mkono wake wa pili, inawasaidia mambo mengi, hasa pale ambapo wameshindwa kufika, wao wanafanya.

"Mmeibua changamoto nyingi ambazo zinatukabili katika maeneo yetu. Kufahamu changamoto ni hatua ya awali ya namna ya kukabiliana na mambo yanayotukabili.

"Lengo likiwa ni kumhudumia mwananchi huyuhuyu, ambaye serikali ina dhamana ya kumhudumia. Ninyi wawakilishi wa kata ya Mabogini, niwapongeze kwa utayari wenu, kutoa muda wenu na kufanya haya mambo ambayo mmeyafanya.

"Mmefanya wasilisho zuri na kwa njia ya kitaalamu. Ni wazi kwamba walimu wenu Agness Rukanga na Happy Maruchu, walifanya kazi kubwa sana kuhakikisha kazi hii inafanyika," alisema.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16, kulawiti na kubaka/kunajisi kwa kundi ni kosa la jinai na adhabu yake ni kifungo cha maisha gerezani.