SIKU 100 OFISINI: Kamishna Mkuu TRA akitaja mambo 10 ya kufanyiwa kazi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:22 PM Oct 21 2024
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Yusuph Mwenda.
Picha:Mtandao
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Yusuph Mwenda.

KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Yusuph Mwenda, ameelezea siku 100 za utumishi wake katika nafasi hiyo huku akisisitiza kuwa mamlaka hiyo inaamini katika kuwa na ushirikiano bora na uhusiano imara na walipakodi bila ya kuhatarisha ulipaji kodi stahiki kwa mujibu wa sheria.

Katika andiko lake la kushukuru, aliloliweka katika ukurasa wake wa mtandao wa Facebook, Kamishna Mwenda anasema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kibali cha kutimiza siku 100, akiwa Kamishna Mkuu wa TRA, baada ya kuaminiwa na kuapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan. 

"Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, kuendelea kuniamini kumsaidia kusimamia uendeshaji wa TRA. Pia ninawashukuru viongozi wote wa serikali, wananchi na walipakodi wote, Mwenyekiti na Bodi ya Wakurugenzi ya TRA pamoja na watumishi wote wa TRA kwa ushirikiano  mkubwa wanaonipa katika kipindi cha siku 100. 

"Kwa pamoja tumethibitisha kwamba tunaweza kuwa na ushirikiano na uhusiano mzuri kati ya TRA na walipakodi, bila ya kuhatarisha ulipaji kodi stahiki kwa mujibu wa sheria kama tulivyofanya," anasema.

 Anasema wanaweza kuongeza makusanyo ya kodi bila migogoro na walipakodi, kama ilivyowezekana katika  makusanyo ya robo mwaka ya kwanza ya (Julai - Septemba 2024) kwa kuongeza asilimia 18 ya makusanyo ya kodi. 

Mwenda ambaye kabla ya kuwa Kamishna Mkuu wa TRA, alikuwa Kamishna wa Mamlaka ya Kodi Zanzibar (ZRA), katika andiko lake hilo, anasema wanaweza kuwatembelea na kuwasikiliza walipakodi wa nchi  nzima (kama walivyotembelea mikoa 25 nchi nzima, ili kuwasikiliza, kutatua migogoro yao ya kikodi kwa wakati pamoja na  kuwa wabunifu wa kutumia mifumo rahisi ya kuwasikiliza, ili kupata mrejesho toka kwa wananchi na walipakodi wote.  

"Tunaweza kuwekeza na kuharakisha ujenzi wa mifumo ya usimamizi wa kodi ya IDRAS na TANCIS ambayo inasomana na mifumo mingine, ili kurahisisha zaidi ulipaji na ongezeko la kodi, pia tunaweza kujenga mifumo ya kusimamia bandari zetu na mipaka yetu vizuri na kuweka mazingira ya ushindani yaliyo sawa, ili kuwezesha biashara na makusanyo ya kodi ya Forodha kuongezeka," anasema.

 Kamishna Mwenda anasema wanaweza kuimarisha huduma za kodi pamoja na matumizi sahihi ya mfumo wa EFD na kuchukua hatua kwa wasiotumia kwa mujibu sheria za kodi, mifumo ya usimamizi wa kodi (EFDMS) na ushirikiswaji walipakodi.  

Alitumia maadhimisho hayo ya siku 100 kazini kueleza kuwa wanaweza kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa njia tofauti zenye tija na zinazoleta matokeo chanya, ikiwamo kuimarisha ukaguzi na uchunguzi, ili kuwatambua na kuwachukulia hatua wachache wanaokwepa kodi, kuleta usawa katika shughuli za kiuchumi nchini.  

"Tunaweza kama TRA kuendelea kuongeza idadi ya walipakodi nchini, kuimarisha utoaji huduma nzuri, kuongeza weledi, ubunifu na uadilifu pamoja na kuwajali wateja wetu, ili kuimarisha ulipaji kodi wa hiari nchini," anasema. 

Anasisitiza TRA itaendelea kushirikiana na wadau wote wa kodi, wakiwamo viongozi wa taasisi na jumuiya za wafanyabiashara nchini, ili kuendelea kujenga na kuimarisha mfumo wa kodi ulio sawa, unaotabirika, unaowezesha ukuaji wa biashara nchini, wenye ufanisi, utatuzi wa migogoro ya kikodi kwa haraka na unaohamasisha wananchi na wafanyabiashara kufurahia kulipa kodi kwa hiari. 

Anatumia kaulimbiu ya 'Pamoja Tunajenga Taifa' kuwashukuru   walipakodi wote na kuwahakikishia TRA itaendelea kutekeleza maagizo yote ya Rais ya kuwasikiliza walipakodi, kuendelea kutoa elimu ya kodi, kuweka mazingira wezeshi ya shughuli za kiuchumi nchini, kuimarisha utoaji huduma za kodi na kuendelea kufanya vizuri zaidi, ili kuiwezesha serikali kutimiza majukumu yake ya kuwaletea maendeleo wananchi.