Viongozi wawili BAVICHA, BAWACHA watimkia CCM

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:51 AM Oct 21 2024
Viongozi wawili BAVICHA, BAWACHA watimkia CCM
Picha: Mtandao
Viongozi wawili BAVICHA, BAWACHA watimkia CCM

MWENYEKITI wa Baraza la Vijana Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA (BAVICHA) Wilaya ya Ngara, Titho Philimon na Mwenyekiti wa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) wilayani hapa, Catherine James wamejiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) na kupokewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho taifa, Mohamed Kawaida.

Wakizungumza wakati wa kuhama chama hicho juzi, viongozi hao walidai  walifikia uamuzi huo kutokana na kuwa katika chama chao bila maendeleo yoyote. 

Mwenyekiti wa BAVICHA, Philimon alisema aliamua kwenda CCM baada ya kuridhishwa na utendaji kazi wa Rais Samia Suluhu Hassan na kuwa hatua hiyo itamuwezesha kuungana na vijana wenzake wa kitanzania zaidi ya milioni 21.3 ili kufikia chachu ya maendeleo. 

Naye Mwenyekiti BAWACHA Wilaya, Catherine alisema amekuwa kiongozi wa chama hicho kwa miaka 20, lakini haoni mafanikio ndani ya chama hicho. 

Aidha, alisema katika muda wake ndani ya chama hicho amejizolea wanachama zaidi ya 5,000 hivyo kumuhakikishia Kawaida kuwa watamfuata CCM na kuwa wote watakuwa tayari kutumika kwa muda wowote iwe mvua au jua, kwa maana wamedhamiria kumuunga mkono Rais Samia, hasa katika miradi mikubwa anayoitekeleza ndani ya wilaya ya Ngara. 

Akiwakaribisha ndani ya CCM, Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Kawaida aliwapongeza viongozi hao na kwa uamuzi wao na kusema kuwa wanaendelea na kauli mbiu yao isemayo wanazima zote wanawasha kijani. 

Katika hatua nyingine, aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuacha kuwabeza viongozi na wasimamizi wa uandikishaji wa daftari la wakazi, kwa ajili ya kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwataka kuwa sehemu ya uhamasishaji wanachama kushiriki hatua zote na siyo kulalamikia juhudi zinazofanywa.