Yaliyojiri 'Dabi' Simba, Yanga katika namba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:45 AM Oct 21 2024
Yaliyojiri 'Dabi' Simba,   Yanga katika namba
Picha:Mtandao
Yaliyojiri 'Dabi' Simba, Yanga katika namba

MECHI ya watani wa jadi, Simba na Yanga ilimalizika Jumamosi iliyopita, kwa Yanga kupata ushindi wa bao 1-0, ambapo beki wa kulia wa 'Wekundu wa Msimbazi', Kelvin Kijili, alijifunga mwenyewe katika harakati za kutaka kuokoa.

Ilikuwa ni mechi ya raundi ya nane ya Ligi Kuu Tanzania Bara, mzunguko wa kwanza iliyochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika makala haya, tunakuletea matukio, takwimu, rekodi na yote ya kusisimua yaliyojiri kwenye mchezo huo, twende sasa... 

86# Ni dakika ambayo Yanga ilipata bao la ushindi kwenye mchezo huo, ambalo beki wa Simba, Kelvin Kijili, alijifunga mwenyewe alipokuwa akijaribu kuokoa. 

70# Ni dakika ambayo beki Chamou Karaboue aliyeingia badala ya Abdurazack Hamza, aliteleza akiwa karibu na lango lake, baada ya kupasiwa mpira na Moussa Camara, mpira ukanaswa na wachezaji wa Yanga, lakini kipa wa Simba akisimama imara na kuokoa. 

64# Ni namba ya mchezo huo kwa mujibu wa Bodi ya Ligi katika mpangilio wao wa michezo yote ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/25. 

42# Ni dakika ambayo Yanga ilifanya shambulio pekee la hatari zaidi katika kipindi cha kwanza, mpira wa Pacome Zouzoua aliurudisha ndani wachezaji wa Simba wakidhani ulikuwa umetoka, ulimkuta Stephane Aziz Ki, aliyepiga shuti kali akiwa karibu na lango, lakini ulidakwa na kipa Camara kisha ukamponyoka na kugonga nguzo ya pembeni, kabla ya kuudaka tena. 

37# Abdulrazack Hamza, angeweza kuipatia Simba bao katika dakika hii, lakini mpira aliounganisha kwa kichwa kutokana na faulo ya Jean Charles Ahoua, ulipaa juu lango,  

29# Namba hii inasimama kama idadi ya michezo ambayo timu hizo zimekutana tangu msimu wa Ligi Kuu 2010/11. 

27# Ni dakika ambayo mchezaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki, alikaribia kuiandikia Yanga bao,  shuti lake lilimbabatiza Fondoh Che Malone, mpira ukampoteza maboya kipa, Camara, lakini bahati nzuri ulitoka nje.

 13# Ni dakika ambayo Yanga ilifika kwa mara ya kwanza kwenye lango la Simba, baada ya wapinzani wao kuanza mchezo huo kwa kasi na kukosa mabao mawili ya wazi dakika za mwanzoni.

 10# Yanga ilichezesha jumla ya wachezaji 10 wa kigeni katika mchezo wao dhidi ya Simba, ambao ni Djigui Diarra raia wa Mali, Yao Kouassi na Pacome Zouzoua kutoka Ivort Coast, Shadrack Boka na Maxi Nzengeli (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Khalid Aucho ambaye ni Mganda, Prince Dube (Mzimbabwe), Stephane Aziz Ki (Burkina Faso), Wazambia Kenneth Musonda na Clatous Chama.

Namba hii pia inasimama kama  idadi ya michezo ambayo Yanga imeifunga Simba kwenye michezo ya Ligi Kuu tangu msimu wa 2010/11.

 9# Idadi ya wachezaji wote wa Simba wa kigeni waliocheza kwenye mchezo wa juzi, nao ni Moussa Camara raia wa Mali, Fondoh Che Malome na Leonel Ateba (Cameroon), Debora Fernandes (Angola), Jean Charles Ahoua na Chamou Karaboue (Ivory Coast), Joshua Mulate (Zambia), Steven Mukwala (Uganda) na Augustine Okajepha wa Nigeria.

 8# Yanga ilianzisha idadi hii ya wachezaji wa kigeni katika mchezo wa jana, ambao ni Djigui Diarra raia wa Mali, Yao Kouassi na Pacome Zouzoua (Ivort Coast), Shadrack Boka na Maxi Nzengeli (DR Congo), Khalid Aucho (Uganda), Prince Dube (Zimbabwe), Stephane Aziz Ki ambaye ni raia wa Burkina Faso.

 7# Jumla ya wachezaji wote wazawa wa Simba ambao walicheza mchezo wa juzi, dhidi ya Yanga ambao ni Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Abdulrazack Hamza, Yusuph Kagoma, Kibu Denis, Kelvin Kijili na Edwin Balua. 

6# Ni idadi ya wachezaji wa kigeni ambao Simba iliwaanzisha katika mchezo wa Jumamosi, nao ni Moussa Camara raia wa Mali, Fondoh Che Malome na Leonel Ateba (Cameroon), Debora Fernandes (Angola), Jean Charles Ahoua (Ivory Coast) na Joshua Mulate wa Zambia. 

5# Idadi ya wachezaji wote wa Yanga wazawa waliocheza mechi ya watani wa jadi dhidi ya Simba Jumamosi, iliyopita ambao ni Dickson Job, Mudathir Yahaya, Ibrahim Hamad 'Bacca', huku Clement Mzize na Bakari Mwanyeto wakiingia kipindi cha pili kutokea benchini. 

4# Leonel Ateba alikosa bao la wazi kwenye dakika hii, alipojaribu kumlamba chenga  Diarra, lakini kipa huyo alikuwa makini na kuondosha hatari.  

3# Namba hii inasimama kwa wachezaji watatu wa Yanga wazawa walioanza mchezo wa dabi, ambao ni Dickson Job, Mudathir Yahaya na Ibrahim Hamad 'Bacca'. 

2# Idadi ya makipa wa kigeni waliodaka mchezo huo, Diarra kwa upande wa Yanga na Camara upande wa Simba. 

1# Bao pekee lilopatikana katika mchezo huo, uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ambalo liliipa Yanga pointi tatu.