TFF, TPLB imetosha, sasa leteni waamuzi wa 'dabi' kutoka nje

Nipashe
Published at 11:53 AM Oct 21 2024
TFF, TPLB imetosha, sasa leteni waamuzi wa 'dabi' kutoka nje
Picha: Mtandao
TFF, TPLB imetosha, sasa leteni waamuzi wa 'dabi' kutoka nje

MECHI ya watani wa jadi, Simba na Yanga imemalizika kwa lawama kutoka kwa mwamuzi, Ramadhani Kayoko, ambaye mbali na wadau wengi wa soka, lakini pia wanachama na mashabiki wa 'Wekundu wa Msimbazi' wanamtuhumu kuwanyima penalti mbili za wazi.

Hii si mara ya kwanza kwa mashabiki wa soka kulalamika juu ya udhaifu wa makusudi au wa bahati mbaya kwenye michezo ya dabi. Kwa miaka ya hivi karibuni waamuzi wa Tanzania wanaonekana kushindwa kabisa kumudu kucheza michezo hii inayozihusu timu hizi.

Wamekuwa wanasita au kuogopa kutoa maamuzi magumu licha ya kwamba makosa yanaonekana wazi. Kwa mfano kwa mechi ya juzi kwa marudio ya televisheni, haikuhitaji wala VAR kujua Kibu Denis alikuwa amechezewa madhambi ndani ya eneo la hatari na wachezaji wa Yanga mara mbili na mwamuzi akapuuzia.

Kwa mtazamo na maoni ya wadau wengi wa soka, wanasema hata adhabu ambayo mwamuzi huyo aliikubali ni kwa sababu tu ilikuwa nje ya boksi na haikupaswa kuwa penalti.

Tumeona mashabiki wa Simba wakilalamika sana na wengine wakiapa kuwa hawatoenda tena uwanjani wala kuangalia mipira vibandani.

Wanadai kuwa kwa mechi za hivi karibuni wamekuwa wakinyimwa haki yao ya kupata penalti, wakikumbushia mchezo uliopita wa Agosti 8, mwaka huu kwenye nusu fainali ya Ngao ya Jamii.

Alikuwa ni Kijili ambaye aliangushwa na Boka, ndani ya boksi ambapo ingeweza kuwapa nafasi ya Simba kusawazisha, lakini mwamuzi Ahmed Arajiga hakutoa adhabu hiyo.

Na juzi imejitokeza hivyo hivyo na wanaamini wamenyimwa, hivyo wanaona kama wao hawana haki ya kutendewa ndani ya dakika 90 kwenye michezo ya dabi.

Tunavyoona, kwa uchezeshaji huu wa waamuzi tutaendelea kupoteza watazamaji wengi uwanja na hata kwenye vibanda umiza na kumbi za starehe ambako hukusanyika kufuatilia mechi hizo.

Siku zote mashabiki wa soka hukubali wanapofungwa, lakini wanapoona wanapoteza kwa namna ambayo wanaonewa huona hakuna maana yoyote ya kuendelea kuweka akili, nguvu na pesa kwa kitu ambacho wanaona haki haitendeki.

Kwa hili tunawaomba Bodi ya Ligi ya TFF (TPLB), iangalie suala hili kwa makini, ikiwezekana waamuzi wa mchezo huu wawe wanatoka nje ya nchi kama ambavyo nchi nyingi za Afrika sasa hivi zinafanya.

Dabi zote kubwa za Afrika kwa sasa waamuzi huwa wanatoka nje ya nchi, kuanzia Misri, Morocco, Tunisia, Algeria hata Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Afrika Kusini.

Kama dabi ya Tanzania ni ya sita Afrika kwa ubora, iweje iendelee kutiwa aibu na doa kupitia waamuzi hawa ambao wanaonekana kushindwa kuimudu? Tunatambua kwa wenzetu waliamua hayo, baada ya kutokea fujo viwanjani na machafuko ambayo mengi yamesababishwa na waamuzi.

Hatutaki kufika huko, hivyo ni vizuri zaidi kuzuia kuliko kutibu, fikiria kwamba mchezo unaofuata, halafu itokee mwamuzi tena awanyime penalti kama hivi huwezi kujua nini kitatokea.

Tunachowashauri TPLB, sasa imetosha, ifanye iwezekanavyo kuwaleta waamuzi kutoka nje ya nchi, hata nchi za jirani tu, kama Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan, Somalia, Eritrea ambako kuna waamuzi bora tu na wengi huchezesha fainali za AFCON na michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Na ikiwezekana wasiwe hata wanatangazwa, kwani si lazima kufanya hivyo. Kama listi ya wachezaji inatolewa dakika chache kabla ya mchezo kuna haja gani ya waamuzi itoke wiki, au siku tatu kabla ya mchezo? 

Hilo likifanyika, tunaamini litapunguza kwa kiasi kikubwa kelele hizi ambazo zinawahusisha waamuzi kuwa vinasaba (DNA) na moja kati ya timu hizo wapopewa dhamana ya kuzichezesha.