Viwanda vya Uchenjuaji Madini kujengwa nchini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:08 PM Apr 23 2024
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amekutana na kufanya mazungumzo wadau wa sekta ya madini ambao wameonesha nia kuanzisha ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji wa madini ya metali ili kuunga mkono jitihada za serikali za kuongeza thamani madini nchini.

Wadau hao ni kutoka Kampuni ya Mineral Access System Limited(MAST) ikiwakilishwa na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Georgefrey Kente pamoja na Mwekezaji kutoka Lithuania, Arunas Sermuksnis ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Akmenite Limited. 

Akizungumza katika mkutano huo,  Mkurugenzi wa Kampuni ya MAST Georgefrey Kente ameonesha utayari wa kampuni yake kujenga viwanda vitatu vya uchenjuaji wa madini ya metali katika mikoa ya Ruvuma,Dodoma na Lindi ambapo ujenzi wake unatarajiwa kuanza mapema mwaka huu na zaidi ya Dola za kimarekani milioni 15 zitatumika kukamilisha ujenzi huo.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Akmenite Limited, Arunas Sermuksnis amehakikishia serikali kwamba wataleta nchini teknolojia ya kisasa ya uchenjuaji wa metali ili shughuli za uongezaji madini kufanyika ndani ya nchi na hatua za awali za uanzishwaji wa kiwanda hicho zimeanza tayari.

Naye,  Waziri  Mavunde amezipongeza Kampuni hizo kwa uamuzi huo wa kuwekeza viwanda vya uchenjuaji madini ndani ya nchi na kuhimiza ukamilishaji wake uwe ndani ya muda mfupi ili wachimbaji wa Tanzania wanufaike na fursa hiyo kwakuwa kwa hivi sasa moja ya changamoto kubwa inayowakabili
Wachimbaji wa madini ya metali ni kukosekana kwa teknolojia ya uchenjuaji ili kutosafirisha madini ghafi nje ya nchi.

Waziri Mavunde pia amewahakikishia wawekezaji hao kwamba serikali kupitia Wizara ya Madini itatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha kwamba uwekezaji huu unafanyika kwa manufaa ya maendeleo ya sekta ya madini Tanzania.