Simba yarejesha majeshi kwa Mpanzu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:19 AM Jul 27 2024
Winga raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Elie Mpanzu.
Picha: Mtandao
Winga raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Elie Mpanzu.

KLABU ya Simba imerudi tena kwenye meza ya mazungumzo na winga raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Elie Mpanzu, baada ya hapo awali kushindikana.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema viongozi wa Simba wameamua kurejea kwa nguvu zote baada ya kutoweka kwa mchezaji wao, Kibu Denis, anayedaiwa kutorokea nchini Norway, bila ruhusa ya waajiri wake.

Chanzo kinasema awali Simba ilipeleka ofa ya dola za Kimarekani 150,000  huku klabu yake ya AS Vita ikitaka dola 250,000 lakini sasa wekundu hao wameongeza pesa kufikia dola 200,000 kumchukua winga huyo.

"Kwa sasa viongozi wanahaha kwa sababu upande wa kushoto kuna Jushua Mutale, kulia alikuwa anategemewa zaidi Kibu, kwa haya yaliyotokea ni kwamba hata akirejea hatoweza kuwa sehemu ya kikosi, hivyo wameamua kurudi sokoni kusaka winga mwingine wa kulia mwenye kiwango cha kimataifa," kilisema chanzo cha taarifa hiyo.

Chanzo kingine kilisema mara hii ya pili mambo yana kwenda vizuri na huenda kuanzia leo Jumamosi anaweza kutangazwa rasmi kuwa mchezaji mpya wa Simba.

Meneja wa mchezaji huyo alijitambulisha kwa jina la Papa Papida, alisema kwa sasa hawezi kuweka kila kitu hadharani kwani kilichopo ni siri kati yake ya klabu ya Simba.

"Kwa sasa jambo hili ni siri yetu na Simba, muwe wa subira kama dili litafanikiwa au halitafanikiwa mtajua tu," alisema meneja huyo.

Alibainisha kuwa kama itampata basi Simba itakuwa na mchezaji mzuri ambaye alikuwa anawaniwa na klabu nyingi barani Afrika.

"Ni mchezaji mzuri sana tangu zamani, ila kwa sasa nyota yake inang'aa, timu nyingi Afrika zinamsaka, najua Simba hawawezi kushindwa kwa sababu ni timu kubwa sana," alisema Papida.

Wakati hayo yakiendelea, habari zinasema kuwa viongozi wa klabu hiyo wameingia tena sokoni kusaka straika baada ya kile kinachoelezwa kuwa Kocha Mkuu, Fadlu Davids kutoridhishwa na uwezo Freddy Michael.

Taarifa kutoka kambini zinasema kocha amewaambia mabosi wa Simba wasake straika mwenye uwezo wa hali ya juu wa kupachika mabao kabla dirisha la usajili kufungwa, Agosti 16.

Wakati huo huo, golikipa  wa timu hiyo, Ali Salim alisema wamejiandaa vizuri kwa msimu ujao na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.

"Tunajiandaa vizuri kwa ajili ya msimu mzima, lakini pia tunaiangalia tarehe 8, kwenye mechi yetu ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga kwani malengo ndiyo yanaanzia hapo, kutwaa mataji, nawataka mashabiki wajitokeze kwa wingi kuiona Simba mpya," alisema.

Katika hatua nyingine, uongozi wa klabu hiyo jana imemtangaza Uwayezu Francois Regis kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu mpya kuanzia Agosti Mosi mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed Dewji 'Mo', inasema kuwa Regis raia wa Rwanda amewahi kushika nyadhifa mbalimbali kwenye sola la nchi hiyo, akiwa pia na ujuzi na uzoefu katika soka, utawala, na fedha.

Regis pia amewahi kushika nyidhifa mbalimbali kwenye shirikisho la soka Rwanda na lile la Afrika, CAF.

Mnyarwanda huyo anachukua nafasi ya Iman Kajula ambaye ametangaza kuachia nafasi hiyo ifikapo Agosti 31 mwaka huu.