MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, wamejadili taarifa mbalimbali kwenye kikao cha baraza cha robo ya pili, kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo ya wananchi na halmashauri hiyo.
Kikao hicho cha Baraza la Madiwani, kimefanyika jana, Februari 6, 2025 katika ukumbi wa mkutano wa halmashauri hiyo na kuhudhuriwa na wananchi.
Mmoja wa madiwani hao, Victor Mkwizu kutoka Kata ya Ngokolo, aliuliza swali la papo hapo, kwamba ujenzi wa kituo cha polisi katika Majengo Mapya, umechukua muda mrefu na kushindwa kukamilika zaidi ya miaka mitano.
Diwani wa Kata ya Ndembezi, Victor Mmanywa, naye aliuliza swali juu ya kusua kukamilika kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Ndembezi, kwamba utakamilishwa lini na ulianzishwa kwa nguvu za wananchi zaidi ya miaka mitano.
Pia, Diwani mwingine wa Vitimaalumu, Pica Chogelo, naye aliuliza swali juu ya upimaji wa viwanja katika Kata ya Mwamalili
Enock Lyeta, Diwani wa Kata ya Oldshinyanga, aliuliza swali kwa niaba ya wananchi tisa kuwa watalipwa lini fidia zao katika eneo la Butulwa.
Diwani wa Kata ya Mwawaza, Juma Nkwambi, naye aliuliza swali juu ya hatua za ujenzi wa Stendi ya Mabasi Mwawaza.
Akijibu maswali hayo, Mchumi wa Manispaa ya Shinyanga, Mensaria Mrema, amesema maboma yote ambayo yalianzishwa kwa nguvu za wananchi pamoja na halmashauri, taarifa zake zimepelekwa TAMISEMI, ili kupewa kipaumbele katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Ofisa Ardhi wa manispaa hiyo, Jacob Mwinuka, akijibu swali la upimaji viwanja eneo la Mwamalili, amesema upimaji wa eneo husikanategemea na uhitaji wa wananchi na kutoa ufafanuzi kwamba, kupitia kwenye kamati zao za maendeleo ya Kata hujadiliwa na kuomba kupimiwa maeneo yao.
Kwa upande wa ulipwaji fidia wananchi katika eneo la Butulwa Oldshinyanga, amesema kwamba tayari fedha zimeshatengwa kwenye bajeti ijayo na kwamba watalipwa.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko, amesema manispaa hiyo itajitahidi kukamilisha maboma ambayo yameanzishwa kujengwa kwa nguvu za wananchi, moja baada ya jingine kupitia fedha za mapato ya ndani.
Amewaagiza pia maofisa watendaji wa Kata, kwamba wanapokuwa wakiandaa taarifa, kwa ajili ya kuwasilishwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani, ili kupitishwa, wawe makini na uandaaji wa taarifa hizo na kusiwepo na mapungufu.
Pia, amemuagiza Mkurungenzi wa Manispaa ya Shinyanga, kuchukua hatua ya kuwaondoa watu ambao wanaishi kwenye eneo la shule ya msingi Lubaga ambao wameweka zizi la ng'ombe.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Revocatus Lutunda, amewapongeza madiwani hao kwa ushiriki mzuri wa kikao hicho cha baraza na kuhoji mambo mbalimbali, kwa ajili ya mustakabaki wa maendeleo ya wananchi.
Aidha, amesema kwa maelekezo ambayo yametolewa kwenye kikao hicho, menejimenti imeyachukua na itayafanyia kazi.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga, Said Kitinga, amesema baraza hilo la Madiwani Manispaa ya Shinyanga, lipo makini na linaendeshwa kwa weledi mkubwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED