Dube, Aziz Kii waahidi makubwa

By Faustine Feliciane ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:27 AM Jul 27 2024
Aziz Kii.
Picha: Yanga SC
Aziz Kii.

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki na mshambuliaji mpya wa klabu hiyo, Prince Dube wameahidi kutoa uwezo wao wote kuisaidia timu hiyo kutetea ubingwa na kufanya vizuri kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kutoka Afrika Kusini, Aziz Ki, alisema kwa aina ya kikosi chao kilivyo sasa hivi anauhakika watafanya vizuri zaidi msimu ujao.

"Nataka kuwa sehemu ya historia ya klabu hii, nitapambana zaidi ya msimu uliopita kuhakikisha tunafikia malengo yetu, kikubwa ni  kuona tunafika mbali zaidi ya msimu uliopita," alisema Azi Ki.

Aidha, Dube ambaye ameanza kuonyesha makali yake kwenye timu hiyo katika michezo ya kirafiki wanayoendelea kucheza Afrika Kusini amesema ataendelea kupachika mabao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, huku akitambulisha ushangiliaji mpya.

Dube aliyesajiliwa kutoka Azam FC, alisema amefurahi kuanza kuifungia timu hiyo goli ambalo limemfanya kujiamini zaidi akiwa na kikosi hicho.

"Kwa muda mrefu sijacheza mechi ngumu, naona taratibu kama muunganiko unaanza kuja, nawasihi wachezaji wenzangu tupambane kwa ajili ya kuwafurahisha Wananchi," alisema Dube.

Katika mchezo dhidi ya TX Galaxy juzi, Dube akiwa ameingia kipindi cha pili, alitumia dakika 10 tu kuupachika mpira ndani ya vyavu na kuipatia Yanga ushindi wa bao 1-0, ukiwa ni ushindi wa kwanza wa timu hiyo tangu itue nchini humo katika michezo ya kimataifa ya michuano maalum.

"Ukiwa mshambuliaji kuna maeneo mengine ukikaa hasa pembeni, mabeki na kipa wa wapinzani wanajua huwezi kupiga, wanadhani utatoa pasi au krosi, sasa 'unawasapraizi', ndicho nilichofanya na huwa nafanya mara kwa mara," alisema Dube akilizungumzia bao alilofunga.

Straika huyo hakucheza kwa kiasi cha miezi sita msimu uliopita kutokana na kuwa na mgogoro wa kimkataba na klabu yake ya zamani, Azam FC, ambapo alikwenda kushtaki Kamati na Sheria na Hadhi za Wachezaji.

Hata hivyo alishindwa kesi hiyo na kulazimika kuilipa Azam kiasi cha Sh. Milioni 500 kilichomfanya kuwa huru na kuamua kujiunga na timu yake ya sasa.