WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema Tanzania inajitosheleza kwa nondo na mabati, hivyo hakuna haja tena kwa serikali na taasisi zake kuagiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Pia ameziagiza taasisi zinazonunua bidhaa za ujenzi kutoka kwa wazalishaji wa ndani kuhakikisha wanalipwa kwa wakati ili wawekeze zaidi na kuongeza ajira nchini.
Alitoa agizo hilo jana Kisemvule, Mkuranga mkoani Pwani, alipotembelea kiwanda cha Lodhia Industries kuona uzalishaji na kusikiliza changamoto za mwekezaji huyo.
Kiwanda cha Lodhia kimewekeza Dola za Marekani milioni 120 kwenye uzalishaji wa nondo, mabati na bidhaa za plastiki na kwa mwezi kinazalisha tani 18,000 za nondo na matarajio ni kuzalisha tani 1,000,000 kwa mwaka.
“Tumeshajitosheleza kwa nondo na si kujitosheleza tu. Nimeshunudia kiwanda cha Lodhia wanatengeneza nondo zenye ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa. Kwa hiyo tununue vya kwetu tuachane na utegemezi wa kuagiza kutoka nje.
“Nnitoe rai kwa taasisi zinazopata zabuni za ujenzi wa miradi mbalimbali ya serikali lazima tuanze kutumia bidhaa zetu zinazozalishwa hapa nchini kwa sababu tumeshuhudia ubora kwa hiyo hatuwezi kuwa na visingizio,” alisema
Prof. Mkumbo alisema moja ya malengo makubwa ya serikali ni kupunguza uagizaji wa bidhaa nje ya nchi kulinda hazina ya fedha za kigeni na kwamba kiwanda cha Lodhia kimekuwa mkombozi kwenye uzalishaji wa shehena ya kutosha ya nondo zinazotumika katika miradi mbalimbali ya serikali.
Alisema kiwanda hicho kimepanuliwa na kuanza kutengeneza malighafi za kutengeneza misumari hatua ambayo alisema ni ya kupongezwa kwani itapunguza utegemezi wa kuagiza malighafi hiyo nje ya nchi.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukiagiza malighafi za kutengeneza misumari na mabati lakini wenzetu hawa wameshaanza kutengeneza malighafi hizi hii ni hatua kubwa sana ya kujivunia kwa maendeleo ya viwanda,” alisema.
Alisema changamoto aliyobaini kwenye ziara yake ni kuwapo kwa uaagizaji wa nondo kutoka nje ya nchi licha ya kiwanda hicho na vingine kuzalisha bidhaa za kutosha na zenye viwango hivyo aliahidi kuchukua hatua.
Alisema kama miradi mikubwa kama ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR na bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Nyerere Hydro Power Project (JNHPP) imetumia bidhaa za ndani zikiwemo nondo hakuwezi kuwa na sababu ya kuendelea kuagiza kutoka nje.
“Kwa kweli kiwanda cha Lodhia kimeisaidia sana serikali kwenye eneo la kuacha utegemezi wa kuagiza bidhaa za nondo kutoka nje kwasababu bila wao tungetumia fedha nyingi za kigeni ndiyo maana naendelea kusisitiza tuthamini na tutumie vya kwetu,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nasri, alisema uwekezaji uliofanywa na kiwanda hicho umekuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa Wilaya hiyo kiuchumi na ajira kwani vijana wengi wamekuwa wakinufaika nacho.
Alisema Lodhia ilianza na kiwanda kimoja cha kuzalisha nondo lakini kimeendelea kujipanua na kuongeza cha kuzalisha bidhaa za plastiki na sasa kinajenga kiwanda cha kuzalisha mabati ambacho kinatarajiwa kuanza uzalishaji mwezi Mei mwaka huu.
“Kiwanda cha mabati cha Lodhia kitakapoanza kazi hivi karibuni vijana wetu 600 watapata ajira hapa kwa hiyo tunashukuru mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo serikali yetu inaendelea kuyaweka na kuvutia wawekezaji,” alisema
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED