Airtel yaweka mikakati kuongeza ufanisi

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 08:33 PM Jul 26 2024
Mkurugenzi wa Airtel Afrika Sunil Taldar.
Picha: Mtandao
Mkurugenzi wa Airtel Afrika Sunil Taldar.

KAMPUNI ya mawasiliano ya Airtel imebainisha kuwa imechukua hatua za uboreshaji wa usanifu wa mtandao na kuanzisha mipango na mikakati ili kupunguza gharama, huku wakihakikisha matarajio ya ukuaji wa siku za usoni yanakuwa endelevu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na kampuni hiyo, wanatarajia manufaa kamili ya hatua hiyo kupatikana mwaka ujao, na kwamba misingi thabiti na utekelezaji uliozingatiwa unaendelea kusaidia utendaji kazi licha ya changamoto za mazingira ya uchumi mkuu.

Aidha, taarifa hiyo imebainisha kuwa kwa robo ya pili ya mwaka huu iliyoishia Juni 30, wamepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuongeza wateja wa mawasiliano hadi milioni 155.4 sawa na asilimia 8.6.

Pia imeongeza wateja wa data milioni 64.4 sawa na asilimia 13.4, huku matumizi ya data kwa kila mteja yakifikia GB 6.5 sawa na 25.1 huku upenyezaji wa simu mahiri ukiongezeka kutoka asilimia 4.7 hadi 41.7.

“Uzoefu wa wateja unabaki kuwa msingi wa mkakati wetu na uwekezaji endelevu wa mtandao unaochochea ongezeko la uwezo na huduma,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Africa, Sunil Taldar, amesema mafanikio hayo yanaonyesha ukuaji endelevu katika msingi wa wateja wao na matumizi, akieleza kuwa utendaji bora huwawezesha kunasa fursa mbalimbali zitakazowawezesha kupiga hatua kwenye tasnia hiyo.

“Kipaumbele muhimu kwetu ni kutafuta fursa mpya za kukua zaidi haswa katika biashara za kituo cha data kote barani Afrika.

“Tutajenga msingi imara ulioanzishwa kwa miaka mingi ili kutoa fursa hizi mpya za biashara. Muhimu zaidi, msisitizo wetu ni kuboresha kwa kiasi kikubwa uzoefu wa wateja,” amesema Sunil.