Feitoto 'kukiwasha' zaidi msimu ujao

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:34 AM Jul 27 2024
 Fei Toto.
Picha: AZAM FC
Fei Toto.

PAMOJA na wadau wengi wa soka kuona mchezaji Feisal Salum 'Feitoto' alikuwa na kiwango bora msimu uliopita, kiungo huyo mshambuliaji amebainisha kwake haukuwa msimu mzuri kutokana na kukabiliwa na presha kubwa ya mambo mbalimbali yaliyomtokea na kuahidi atakuwa bora na kukiwasha zaidi msimu ujao.

Akizungumza akiwa nchini Morocco ambako yuko kambini na kikosi chake cha Azam FC, Fei Toto, alisema alikuwa na msimu bora kitakwimu, lakini kwake ulikuwa msimu wenye presha nyingi kwani kila mtu alitaka kuona nini anafanya kwenye timu yake mpya.

"Pamoja na kufanya vizuri, lakini msimu uliopita ulikuwa mgumu sana kwangu ulikuwa na presha sana na yote yaliyotokea, lakini yote nimepita salama, sasa nimetulia, nadhani nitakuwa bora zaidi ya msimu uliopita ingawa najua ligi na mashindano yote yatakuwa magumu sana," alisema Feitoto.

Feitoto, alisema amejiandaa vizuri na lengo lake kubwa siyo kuwa mfungaji bora au tuzo binafsi bali kuisaidia timu yake ili ifikie malengo yaliyokusudiwa ambayo ni kutwaa taji la Ligi Kuu.

Fei Toto pia alisema anajisifia faraja kubwa kuteuliwa kuwania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka na kiungo bora kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

 "Najisikia faraja kubwa kuteuliwa kuwania tuzo hizo, napenda kuwashukuru pia wachezaji wenzangu na benchi la ufundi kwa sababu hao wote ndiyo walionifanya kuwa bora hadi kuteuliwa, kilichobaki ni kuiachia Kamati ya Tuzo ifanye kazi yake, tusiwaingilie kwenye majukumu yao," alisema kiungo huyo wa zamani wa Yanga.