Vijana waitwa kufuga nyuki

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 11:23 AM Dec 31 2024
Ufugaji nyuki.
Picha:Mtandao
Ufugaji nyuki.

VIJANA wametakiwa kuitumia misitu kwenye shughuli za ufugaji nyuki badala ya kupoteza muda kutembea mijini na barua za kuomba kazi, jambo ambalo linawachelewesha kufikia malengo yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kijiji cha Nyuki, Philemon Kiemi, alisema hayo juzi wakati akizungunza na wanafunzi waliosoma katika Shule ya Sekondari ya Mwenge iliyopo Manispaa ya Singida kuanzia 1991-1994.

Alisema hivi sasa ajira serikalini ni ngumu hivyo vijana wanapaswa kutumia fursa hiyo ya msitu iliyopo nchini kwenye ufugaji nyuki.

"Vijana wanaotembea na barua katika miji kama Dodoma, Dar es Salaam, Arusha na maeneo mengine nawashauri watembelee misitu waione fursa, waone misitu kama ofisi badala ya kutembea na barua kutafuta kazi huko ni kupoteza muda," alisema.

Kiemi ambaye ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) mwaka 2012, alisema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2024 watalii zaidi ya 6,000 wametembelea kijiji cha nyuki kufanya utalii na kujifunza ufugaji wa nyuki ambapo kati ya hao 1,700 wametoka nje ya nchi.

Alisema katika kipindi hicho wananchi zaidi ya 4,800 kutoka katika vijiji na kata zote za Mkoa wa Singida wamepewa mafunzo ya ufugaji nyuki na vifaa vinavyotumika katika ufugaji huo ikiwamo mizinga hatua ambayo itaongeza uzalisha wa mazao ya nyuki hususani vumbi la Singida.

"Naishukuru serikali kwa kuweka mazingira mazuri ambayo yametuwezesha sisi vijana kuingia kwenye biashara ya ufugaji nyuki na kujipatia kipato ambapo mazao yatokanayo na nyuki yanapata soko vizuri ndani na nje ya nchi," alisema.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi waliosoma Shule ya Sekondari ya Mwenge, Emmanuel Hanai, alisema uwekezaji uliofanyika katika kijiji cha nyuki ni mzuri na unavutia watu wengi kwenda kutembelea na kujifunza.

Hanai ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Washauri Elekezi wa Mazingira Tanzania (TEEA), alisema serikali itie mkono kuwasaidia vijana waliojikita katika biashara ya ufugaji nyuki kwa kuhakikisha mazao yanazalishwa yanapata soko ndani na nje ya nchi ili kuinua uchumi wao.