MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Victoria na mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Taifa, Ezekia Wenje, amesema migongano inayoonekana kati ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, na Makamu wake, Tundu Lissu, inachochewa na wapambe, huku akisisitiza kuwa viongozi hao wako sawa.
Akizungumza leo jijini Mwanza wakati wa kuchukua na kurejesha fomu ya kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti Taifa, Wenje amebainisha kuwa maneno ya matusi yanayoenezwa kwenye mitandao ya kijamii yanatokana na wapambe wa pande mbalimbali, lakini viongozi hao wanaendelea kushirikiana kwa maslahi ya chama.
Aidha amewataka wafuasi wake kutumia kauli za staha katika kujenga hoja na siyo matusi kwani kuna maisha baada ya uchaguzi huo.
"Tafadhari wale wanaotukana viongozi na wagombea wekeni akiba ya maneno kuna maisha baada ya Januari, 21. Na hata kama unaniunga mkono mimi usitukane mwingine," amesisitiza Wenje.
Kuhusu kauli yake ya Wananchi wasiokuwa na vyeo ndani ya chama hicho kuwa ni wakunja ngumi, Wenje amesema msemo huo umekuwa ukitumiwa kama utani kwa Wanachama ndani ya chama hicho ukimaanisha nguvu ya umma kama ilivyokauli mbiu ya chama hicho.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED