Mwinyi: Tutabomoa nyumba zilizochakaa, kuzijenga upya

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 10:22 AM Jan 05 2025
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akimkabidhi funguo, Said Hamad Ramadhani, ni mmoja wa wananchi walionunua nyumba za Shirika la Nyumba Zanzibar, wakati wa hafla ya uzinduzi wa nyumba hizo
Picha: IKULU
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akimkabidhi funguo, Said Hamad Ramadhani, ni mmoja wa wananchi walionunua nyumba za Shirika la Nyumba Zanzibar, wakati wa hafla ya uzinduzi wa nyumba hizo

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema nyumba nyingi zilizojengwa na mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar baada ya mapinduzi ya mwaka 1964, zimechakaa na hivyo serikali yake itahakikisha inazibomoa na kuzijenga upya.

Ametaja baadhi ya nyumba hizo zilizojengwa na mwasisi wa mapinduzi ambaye pia ni Rais kwa Kwanza wa Zanzibar, Shekhe Abeid Amani Karume, ni nyumba za Kikwajuni na Kilimani.

Dk. Mwinyi alisema jana kuwa serikali itaendelea kujenga nyumba za kisasa ili wananchi wapate makazi bora na kuyaendeleza maono ya mwasisi huyo katika kuwapatia wananchi maendeleo.

Ni wakati akifungua nyumba za makazi na biashara huko Mombasa, mkoa wa Mjini Magharibu Unguja, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema licha ya nyumba hizo zilizojengwa baada ya mapinduzi kuwa chakavu, miundombinu yake poa imeshaharibika, ikiwamo mifumo ya maji, hivyo serikali itahakikisha inajenga maeneo hayo.

Alisema serikali pia itajenga nyumba 3,000 katika eneo la Chumbuni, Unguja; nyumba 500 Kikwajuni na majengo hayo yakishakamilika, wananchi watapata mazingira mazuri ya makazi.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuna uhitaji mkubwa wa nyumba za makazi na serikali itaendelea kulipa fidia kwa wananchi wote wa Zanzibar ambao wanapisha miradi ya maendeleo na kushauri watu hao wajengewe nyumba za kisasa kama fidia kwa ajili ya nyumba zao.

Hivyo, aliwasisitiza wananchi kutunza miundombinu hiyo na miundombinu mingine na kuweka mazingira safi ili nyumba hizo kuwa na haiba nzuri na zidumu kwa muda mrefu.

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Rahma Kassim Ali, alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa miongozo na maelekezo yake na kufanikisha mradi huo.

Alisema bado wanahitaji fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kutokana na uhitaji mkubwa wa nyumba ili kuendelea kuleta maendeleo hasa katika sekta ya makazi.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Khadija Khamis Rajab alisema ujenzi wa nyumba hizo za makazi 72 umetekelezwa na kampuni Simba Developar chini ya Mshauri Elekezi Wakala wa Majengo Zanzibar. Ujenzi wake ulianza rasmi Mei 15, 2023 na kukamilika rasmi Oktoba 31, 2024, siku ya mwisho ya mwaka jana.

Alisema eneo hilo lina jumla ya block nne na kila block ina nyumba za makazi 18 na maduka ya biashara ambapo hadi kukamilika kwake, zaidi ya Sh. bilioni tisa zimetumika. Hizo ni fedha za mkopo kutoka Serikali Kuu na tayari nyumba zote zimeshapata wanunuzi.

Alisema tayari watu 29 wameshakamilisha malipo na watakabidhiwa funguo zao na 43 wanaendelea na malipo.