Mapaparazi tuombeane Heri ya Mwaka mpya, lakini…!

By Joseph kulangwa , Nipashe
Published at 02:05 PM Jan 03 2025
news
Mchoraji:Msamba
Mapaparazi tuombeane Heri ya Mwaka mpya, lakini…!

JAMANI wasomaji na mashabiki wa safu hii, nakutakieni heri ya mwaka mpya wa 2025. Ilikuwa ni safari ndefu ya milima na mabonde yenye mbu na kila aina ya bughudha za kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Tuwaombee waliotangulia mbele za haki, tuwaombee walio na maumivu ili Mungu awape afueni warejee kulijenga Taifa lao, tuwaombee wanaotaka kutuongoza, wajipange vema ili mwaka huu tupate viongozi wazuri zaidi kuliko waliopo. 

Nasema hivyo, kwani ni shauku ya kila mmoja wetu kupata viongozi stahiki wanaoweza kutuvusha kutoka lindi la umasikini lililotulalia hivi sasa na kukosa kufurukuta, kutokana na baadhi ya viongozi wetu kutumia migongo yetu kujinufaisha.

 Nikirejea kwa wenzangu mapaparazi, ni mwaka wa kujisahihisha, kujirekebisha na kuachana na uchawa uliotamalaki miongoni mwetu, ukatupofusha na kushindwa kutazama tulikokanyaga na twendako. 

Tumeshuhudia vyombo vya habari, baadhi vikishindwa kusimamia maadili na kujikuta vimevishwa na kukubali vilemba vya ukoka na kudhani vinakwenda vyema kumbe segemnege. 

Hivi sasa si siri, tuna utitiri wa vyombo hususan magazeti yasiyo na kichwa wala miguu, yanayoandika chochote kinachojitokeza mbele ya waandishi au waandikaji wao, ili mradi kinatekenya wachache, huku yakishindwa kutambua umasikini uliotamalaki kwenye jamii. 

Tumemkaribisha hivi karibuni mwanahabari mwenzetu na mwanasheria nguli, Profesa Palamagamba Kabudi kwa mikono miwili, tukiamini ataturudisha mstarini tulikokwishakengeuka na kukaa pembeni kipindi kirefu sasa. 

Tukimpa ushirikiano wa dhati, Inshallah, atatuvusha na kurejea tulikokuwa enzi hizo, tukiitwa waandishi wa habari au wanahabari, ‘aka’ Mhimili wa Nne wa Dola (kama ni kweli), na kuisaidia nchi kuona iliko na iendako. 

Ni jambo la kushangaza na kusikitisha, kuwa hivi sasa tasnia ya habari imevamiwa, imeingiliwa kinyume cha kawaida na watu wasio na taaluma, ili mradi ni maarufu kwa futuhi na mambo mengine ya kichawachawa. 

Hali ni mbaya zaidi katika vyombo vya kielektroniki, waliko watu wanaosingiziwa kuwa watangazaji, wanaosema chochote bila kujali msikilizaji anataka nini, ili mradi sema yao inawapa umaarufu mitaani, huku wakijiita majina bandia. 

Ni wapi ulisikia taarifa ya habari inasomwa na mtu aliyejipachika jina bandia na watu wakamsikiliza kwa sababu tu eti ni msanii wa futuhi na vichekesho?  

Tanzania hivi sasa inawezekana, ambako wasanii hukana majina yao ya kuzaliwa na kujipachika ya bandia.

Kama nilivyonena hapo juu, tuna magazeti lukuki yanayoandikwa na watu wachache, mtu mmoja anaandikia magazeti hata 10, stori ile ile na sentensi ile ile katika magazeti yote na hakuna anayejali, ili mradi yanatoka, ingawa mengi ya mitandaoni.

 Hivi sasa kuna magazeti yanatoka ukurasa mmoja tu wa mbele, kama bango, lakini yanaungwa mkono na kushangiliwa na wenye mamlaka na kuonekana nayo miongoni mwa yanayoheshimika na kutajwa, ikiwezekana hata ruzuku yapewe. Ni ya kimkakati hayo! 

Kuna vituo vya redio, visivyo na wajuzi na wataalamu wa habari, lakini vipo vinarusha matangazo kwa kutegemea vyombo vingine makini.  

Mathalan, kituo kinakuwa na ‘Kipindi cha Magazeti’, watangazaji wake ambao wengi ni watu wa futuhi, wanachukua magazeti na kusoma ‘lidi storis’ za wenzao ‘font fedi’ na kugeuza zao.  

Ni uvivu na umbumbumbu wa taaluma, ukiwazuia kujitafutia stori zao wakazisoma na kuzijadili! 

Wakiruhusiwa kusoma vichwa vya habari, wao wanasoma habari yote na hata msikilizaji aliyekuwa na shauku ya kununua gazeti hatafanya hivyo tena na badala yake ‘buku’ lake, atalihamishia kununua mafuta ya taa kwa kuwa umeme nao hauaminiki bado. 

Hiyo ni sawa na wafanyabiashara jirani; mmoja anauza vitumbua, mwingine viazi vya kuchemsha, huyu wa viazi ataachana na viazi vyake na kuamua kujadili vitumbua vya mwenzake huku akilalamikia sukari na mchanga na hatimaye kumkatisha tamaa mteja asinunue, hivyo hasara kwa mchoma vitumbua.

 Ikumbukwe tu, akiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, alipiga marufuku usomaji wa aina hiyo, ulioathiri vibaya mauzo ya magazeti na kusababisha malalamiko ya wamiliki.  

Ina maana kila zama na kitabu chake, kwamba Mwakyembe alipoondoka akaondoka na agizo lake? Hapana! Tujirekebishe wahusika. 

Tusimlazimishe Profesa Kabudi ashike mjeledi atushikishe adabu.Chakabhugane!